03 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Nilikuwa na deni la swawm ya Ramadhaan na siwezi kuilipa isipokuwa katika Sha´baan.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth inajulisha kuwa ambaye amekula katika Ramadhaan kutokana na udhuru kwamba analazimika kulipa na kwamba si lazima kulipa kwa haraka. Bali ulazima wake unaweza kucheleweshwa. Inafaa kwa ambaye anadaiwa baadhi ya siku za Ramadhaan akachelewesha kulipa mpaka Sha´baan, hilo ni kutokana na maneno yake ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa). Ingelikuwa haifai kuchelewesha basi asingefanya hivo (Radhiya Allaahu ´anhaa) na akalazimiana nalo. Kwa sababu udhahiri ni kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiyaona hayo.

Lakini kuharakisha kulipa deni ni bora kuliko kuchelewesha. Udhahiri wa kitendo cha ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ni kutanguliza uharakishaji. Kwa sababu ametoa udhuru wa kuchelewesha kulipa kwa sababu ya kutoweza. Endapo angeliweza basi asingechelewesha mpaka Sha´baan.

Jengine ni kwamba kuharakisha kulipa kunatakasa dhimma na kuchukua tahadhari katika dini. Pengine mtu akasahau na khaswa ikiwa masiku ni machache. Aidha kuharakisha kulipa kunaingia katika zile dalili za jumla kuhusu mtu kuharakia matendo mema. Amesema (Ta´ala):

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ

“Kimbilieni msamaha kutoka kwa Mola wenu na Pepo upana wake ni wa mbingu na ardhi imeandaliwa kwa wenye kumcha Allaah.”[2]

أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ

“Hao wanayakimbilia katika mambo ya kheri, na wao ndio wenye kuyatanguliza.”[3]

Si lazima kulipa kwa kufululiza. Bali inafaa kulipa kwa kufululiza na kuachanisha masiku. Amesema (Ta´ala):

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[4]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Hapana vibaya kuachanisha.”[5]

Ni bora kwa ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia kuharakisha kulipa deni lake. Ni kuharakisha kudondosha faradhi na kutoka nje ya makinzano ya wale ambao wamewajibisha kulipa kwa kufuatanisha. Jengine kunampa uchangamfu mfungaji akilipa siku anazodaiwa kwa kufuatanisha tofauti na pale anapolipa kwa kuachanisha na khaswa ikiwa ni masiku mengi anayotakiwa kulipa. Mwaka mzima ni kielezi cha kulipa deni la Ramadhaan kutokana na ueneaji wa Aayah. Isipokuwa tu yale masiku ya ´iyd mbili na masiku ya Tashriyq. Si sahihi kufunga masiku hayo kwa sababu kumekatazwa kufunga.

[1] al-Bukhaariy (1950) na Muslim (1146).

[2] 03:133

[3] 23:61

[4] 02:184

[5] al-Bukhaariy (04/188) kwa cheni ya wapokezi pungufu na ´Abdur-Razzaaq (04/243) kwa cheni ya wapokezi yenye kuungana, Ibn Abiy Shaybah (03/33-34), ad-Daaraqutwniy (02/192). Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Kuna Aathaar kutoka kwa Salaf kuhusu suala hilo zinazoonyesha kufaa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 90-91
  • Imechapishwa: 12/03/2023