05. Bidii kubwa katika ´ibaadah pamoja na hivo wanakhofu

Miongoni mwa mambo ya kusitikisha ni kuwa baadhi ya watu katika Ramadhaan wanafanya ´ibaadah kwa aina mbalimbali ya matendo mema ambapo wanachunga kuswali vipindi vitano vya swalah ndani ya misikiti, wanakithirisha kusoma Qur-aan na wanatoa swadaqah kutokana na mali zao. Ramadhaan inapomalizika wanazembea kufanya matendo mema. Bali pengine wakaacha mambo ya wajibu kama vile swalah za mkusanyiko kwa ujumla na khaswa Fajr, wakafanya mambo ya haramu kama kulala wakati wa swalah, kujishughulisha na nyimbo na muziki na kujisaidia kwa neema za Allaah katika kumuasi. Matokeo yake wakayabomoa waliyoyajenga na wakavunja waliyoyafunga. Hii ni dalili ya kunyimwa na alama ya khasara. Tunamuomba Allaah usalama na uimara.

Salaf walikuwa wakijitahidi kutimiza kitendo, kukikamilisha na kukifanya sanifu. Baada ya hapo wanatilia umuhimu kikubaliwe na wanaogopa kisije kurudishwa nyuma. Miongoni mwa maneno yaliyopokelewa kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ni yeye kusema:

“Tilieni umuhimu mkubwa juu ya kukubaliwa kitendo kuliko mnavyotilia umuhimu ufanyaji wa kitendo chenyewe. Hukumsikia Allaah (Ta´ala) akisema:

إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّـهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ

“Hakika si venginevyo Allaah anatakabalia wachaji Allaah.”?[1]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Aayah isemayo:

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ

“Ambao wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinakhofu.”[2]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) akauliza: “Je, ni wale wanaokunywa pombe na kuiba?” Akamjibu:

“Sivyo, ee msichana wa as-Swiddiyq. Lakini ni wale wanaofunga, wanaoswali na wanatoa swadaqah pamoja na hivyo wanaogopa wasije kukubaliwa:

ولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ

“Hao wanakimbilia katika mambo ya kheri na wao ndio wenye kuyatanguliza.”[3]

Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] 05:27

[2] 23:60

[3] 23:60 at-Tirmidhiy (3175), Ibn Maajah (4198), Ahmad (42/156), Ibn Jariyr at-Twabariy (18/26) na al-Haakim (02/393) ambaye amesema:

“Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”

adh-Dhahabiy akamkalia kimya. Cheni ya wapokezi wake imekatika. Lakini inatiwa nguvu na Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambayo at-Tirmidhiy ameiashiria. Tazama “as-Silsilah as-Swahiyhah” (162).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 88
  • Imechapishwa: 11/03/2023