Imaam ´Abdul-Ghaniy bin ´Abdil-Waahid al-Maqdisiy (Rahimahu Allaah) amesema:

199 – Sahl bin Sa´d as-Saa´idiy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Waja hawatoacha kuwa katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha kukata swawm[1] na wanachelewesha daku.”[2]

Haya yanafahamisha mapendekezo ya kuharakisha kukata swawm na kwamba Ummah utaendelea kuwa juu ya kheri muda wa kuwa wanachunga jambo hili na kuharakisha pindi jua linapozama. Hii ndio Sunnah wakati jua linapozama basi mtu aharakishe kukata swawm. Imepokelewa katika Hadiyth nyingine amesema (Jalla wa ´Alaa):

“Waja wanaopendeza zaidi kwangu ni wale wanaoharakisha kukata swawm.”[3]

Vivyo hivyo daku inatakiwa kucheleweshwa mpaka mwishoni mwa usiku. Hivi ndivo bora daku icheleweshwe mpaka mwishoni mwa usiku, kama ilivyotangulia katika Hadiyth ya Zayd bin Thaabit ya kwamba walikula daku pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anas akaulizwa:

“Kulikuwa kuna kitambo gani kati ya adhaana na daku?” Akasema: “Kiasi cha kusoma Aayah khamsini.”[4]

Bi maana alikuwa akichelewesha daku (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka mwishoni mwa usiku. Daku ni Sunnah iliyokokotezwa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuleni daku. Hakika katika daku kuna baraka.”

Ni Sunnah kwa mfungaji aile mwishoni mwa usiku ili aweze kupata nguvu ya kumtii Allaah.

Bora ni kucheleweshwa daku na kuharakisha kukata swawm. Hii ndio Sunnah.

[1] al-Bukhaariy (1957) na Muslim (1098).

[2] Ahmad (21312). Ameipa nguvu al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (1773).

[3] Ahmad (7241), at-Tirmidhiy (700) na Ibn Khuzaymah (2062). Ameisahihisha Ibn Hibbaan (04/558), al-Bayhaqiy (04/237). Ni dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan-it-Tirmidhiy” (01/80) na katika “Dhwa´yf-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (01/163)).

[4] al-Bukhaariy (1921) na Muslim (1097).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ifhaam fiy Sharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/410-411)
  • Imechapishwa: 21/03/2022