Imaam ´Abdul-Ghaniy bin ´Abdil-Waahid al-Maqdisiy (Rahimahu Allaah) amesema:

198 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Kuna mwanamume alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mama yangu amekufa na juu yake ana funga ya mwezi mzima. Je, nimlipie?” Akamuuliza: “Endapo mama yako angelikuwa na deni ungemfungia?” Akajibu: “Ndio.” Ndipo akasema  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Basi deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Kuna mwanamke alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mama yangu amekufa na juu yake ana swawm ya nadhiri. Je, nimfungie?” Akamuuliza: “Unaonaje iwapo mama yako angelikuwa na deni ambapo ukamlipia si ingelihesabika?” Akajibu: “Ndio.” Ndipo akasema  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Basi mfungie mama yako.”[2]

199 – Sahl bin Sa´d as-Saa´idiy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu hawatoacha kuwa katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha kukata swawm[3] na wanachelewesha daku.”[4]

200 – ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Usiku ukija hapa [mashariki] na ukaondoka mchana hapa [magharibi] na likazama jua, basi amekwishafungua mfungaji.”[5]

MAELEZO

Hadiyth tatu hizi zote zinahusiana na swawm. Ni dalili inayojulisha kuwa mwanamme akifa au mwanamke akifa ilihali anadaiwa swawm ya nadhiri, kafara au Ramadhaan ambayo hakufunga na akaweza kulipa lakini asifanye hivo, basi atafungiwa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kwa kuenea na kwa kuachia na hakuuliza kama ni nadhiri au sio nadhiri na wala hakupambanua. Kwa hiyo ikafahamisha ya kuwa ambaye atakufa ilihali anadaiwa funga basi atafungiwa. Hadiyth hii inapewa nguvu na Hadiyth iliotangulia ya ´Aaishah:

“Mwenye kufa na juu yake yuko na swawm basi afungiwe na walii wake.”

Ni yenye kuenea inahusu swawm ya nadhiri, swawm ya kafara na swawm ya Ramadhaan. Hapa ni pale ambapo mtu atapuuza na asilipe mpaka akafa. Lakini akifa ndani ya maradhi yake au katika safari yake ni mwenye kupewa udhuru. Kama mfano wa Ramadhaan lakini akachelewesha kufunga pasi na udhuru. Katika hali hiyo atalipiwa kutokana na Hadiyth hii Swahiyh na nyenginezo zilizopokelewa zikiwa na maana kama hiyo.

Mwenye kusema kuwa inahusu nadhiri peke yake maoni yake ni dhaifu. Ni yenye kuenea na inakusanya nadhiri, kafara na swawm ya Ramadhaan. Inafahamisha haya yale yaliyotangulia pale aliposema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kufa na juu yake yuko na swawm basi afungiwe na walii wake.”

Ingelikuwa maalum basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angelibainisha. Hakika yeye ndiye kiumbe mfaswaha zaidi na ambaye zaidi anawatakia viumbe mema (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Ni jukumu lake kufikisha. Ingelikuwa inahusu swawm ya nadhiri peke yake basi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angelibainisha. Haya yanatiliwa nguvu na yale yaliyothibiti katika Musnad ya Ahmad kupitia Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba kuna mwanamke alisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Mama yangu amekufa na anadaiwa deni la Ramadhaan. Nimfungie?” Akasema: “Mfungie.”

[1] al-Bukhaariy (1953) na Muslim (197).

[2] Muslim (1148).

[3] al-Bukhaariy (1957) na Muslim (1098).

[4] Ahmad (21312). Ameipa nguvu al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (1773).

[5] al-Bukhaariy (1954) na Muslim (1100).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ifhaam fiy Sharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/408-410)
  • Imechapishwa: 21/03/2022