388 – Rabiy´ah bin Ka´b (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nilikuwa namfanyia kazi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa mchana. Inapofika jioni basi nakwenda mlangoni mwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nikalala hapo. Siachi kumsikia akisema:

سبحان الله، سبحان الله، سبحان ربي

“Allaah ametakasika na mapungufu. Allaah ametakasika na mapungufu. Mola wangu ametakasika na mapungufu.”

Mpaka nikachoka au usingizi ukanichukua. Siku moja alisema: “Ee Rabiy´ah! Omba kitu nikupe.” Nikasema: “Hebu wacha nifikirie.” Nikakumbuka kuwa dunia itakwisha na kumalizika, hivyo nikasema: “Ee Mtume wa Allaah, nakuomba uniombee kwa Allaah anikinge kutokana na Moto na aniingize Peponi.”  Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyamaza, kisha akasema: “Ni nani amekuamrisha kufanya hivo?” Nikasema: “Hakuna yeyote aliyeniamrisha, lakini mimi nimejua kuwa dunia itakwisha na kumalizika na wewe uko na nafasi mbele ya Allaah, hivyo nikapenda uniombee kwa Allaah.” Akasema: “Nitafanya hivo. Hakikisha na wewe unanisaidia kusujudu kwa wingi.”[1]

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” kupitia kwa Ibn Ishaaq. Tamko ni lake. Muslim na Abu Daawuud wameipokea kwa kifupi zaidi. Tamko la Muslim linasema:

“Nilikuwa nalala na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo nikimletea maji ya kutawadhia na mahitaji yake mengine. Akanambia: “Niombe.” Nikasema: “Nakuomba kuambatana na wewe Peponi.” Akasema: “Kingine?” Nikasema: “Ni hayo tu.” Ndipo akasema: “Basi hakikisha unanisaidia kusujudu kwa wingi.”[2]

[1] Swahiyh kupitia zingine.

[2] Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/278-279)
  • Imechapishwa: 26/11/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy