06. Fadhilah za msamaha na kuomba du´aa mwishoni mwa usiku

04 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Katika kila usiku Mola wetu (Tabaarak wa Ta´ala) hushuka katika mbingu ya chini ya dunia pale kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku na anasema: “Nani anayeniomba Nimuitikie? Ni nani anayeniuliza Nimpe? Ni nani anayenitaka msamaha Nimsamehe?”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth inafahamisha juu ya fadhilah za du´aa, kuuliza na kuomba msamaha mwishoni mwa usiku na kwamba du´aa katika kipindi hicho ni yenye kuitikiwa pindi kunapotimia masharti na kukaondoka vikwazo. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) ameahidi kumuitikia yule mwenye kumuomba, kumjibu anayemuuliza na msamaha kwa mwenye kumuomba msamaha.

Allaah amewasifu waja Wake waumini ambao wataingia Peponi na kudumishwa humo milele. Miongoni mwa sifa zao zilizotajwa ni kuomba msamaha mwishoni mwa usiku kabla ya alfajiri. Amesema (Ta´a):

وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ

“… na waombao msamaha kabla ya alfajiri.”[2]

وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ

“… na kabla ya alfajiri wakiomba msamaha.”[3]

Wakati huu mja anatakiwa – na khaswa katika lile kumi la mwisho la Ramadhaan – ajinufaishe na wala asiupoteze kwa kupumbaa, kulala na uvivu. Hichi ni kipindi ambacho Mola anashuka vile inavyolingana na utukufu na ukubwa Wake pasi na kumfanyia namna wala kumfananisha. al-Qahtwaan amesema katika “an-Nuuniyyah”:

Allaah anashuka kila usiku

Katika mbingu ya chini na si kwa siri

na husema: “Ni nani mwenye kuomba nimuitikie?”

kwani hakika mimi niko karibu namuitikia mwenye kuniita

Hashaa kuifanyia namna dhati ya Mola

Namna na ufananishaji ni mambo yenye kukanushwa

Katika nyusiku hizi zilizobarikiwa wakati wa usiku muumini anakusanyikiwa na wakati wa kukubaliwa du´aa, kushuka kwa Mola, kusujudu na utukufu wa zama ambayo ni Ramadhaan. Salaf walikuwa wakilazimiana na jambo la kusimama usiku na khaswa katika mwezi wa Ramadhaan kwa ajili ya kumuigiliza Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakika ndani ya usiku kuna saa ambayo hakuna mtu muislamu anayoafikiana nayo ambaye anamuomba Allaah (Ta´ala) kheri yoyote katika mambo ya kidunia na Aakhirah, isipokuwa Allaah humpa. Hilo linakuwa katika kila usiku.”[4]

Kwa hivyo ni lazima kwa muumini kupupia swalah ya usiku na ahakikishe sababu za yeye kuitikia kwa du´aa kukiwemo kumtakasia nia Allaah, kuhudhurisha moyo, nguvu ya matarajio, kujikurubisha kwa Allaah kwa kufanya matendo mema na maendo yanayopendeza.

[1] al-Bukhaariy (1145) na Muslim (758).

[2] 03:17

[3] 51:18

[4] Muslim (757).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 67-69
  • Imechapishwa: 04/03/2023