06. Allaah alimtuma Nuuh kwa watu pindi walipopetuka kwa watu wema

Allaah alimtuma kwa watu wake walipopetuka mipaka watu wema; Wadd, Suwaa´, Yaghuuth, Ya´uuq na Nasr.

MAELEZO

Kupetuka ni kuvuka mpaka. Kuvuka mpaka kwa watu wema ni kule kuitakidi kuwa wananufaisha au wanadhuru badala ya Allaah.

Wadd, Suwaa´, Yaghuuth, Ya´uuq na Nasr ni majina ya waja wema katika watu wa Nuuh waliokufa katika mwaka mmoja. Watu wao wakawahuzunikia sana. Hapo ndipo walijiwa na shaytwaan na akawaambia watengeneze picha zao na waziweke katika vikao vyao ili waweze kukumbuka hali zao na ziweze kuwapatia uchangamfu wa kufanya ´ibaadah. Aliwajia kwa njia ya kuwapa nasaha ilihali lengo lake ni kutaka kuwaangamiza. Akawahadaa kwa hila kama hii na wakaizingatia kuwa ni njia sahihi kwa kuwa inawapa uchangamfu wa ´ibaadah. Hapa kuna matahadharisho ya fitina ya picha na fitina za kupetuka kwa watu wema. Watu hawa wao waliangalia sehemu ya manufaa na hawakuzinduka juu ya yale madhara yanayopelekea. Haifai kwa mtu akaangalia sehemu ya manufaa na akasahau madhara makubwa yanayopelekea huko katika mustakabali.

Watu wa Nuuh wakaangamizwa kwa mafuriko na masanamu haya yakawa yamepotea mpaka kulipokuja kipindi cha mfalme mmoja shaytwaan wa kiarabu ambaye inasemekana alikuwa akiitwa ´Amr bin Luhayy al-Khuzaa´iy. Mtu huyu yeye ndiye alikuwa ameshika uongozi Hijaaz. Mwanzoni alikuwa ni mwanaume aliyeshikamana na dini ya watu wake. Akapata safari ya kwenda Shaam kwa ajili ya matibabu. Hapo ndipo akakutana watu wa Shaam wanaabudu masanamu ambapo akaingiwa akilini mwake na kitu hichi. Akarudi kwa watu wa Hijaaz na kisiwa cha waarabu na akawalingania katika shirki. Shaytwaan akaja na kumwelekeza sehemu yalipo yale masanamu ambayo yalikuwa yakiabudiwa na watu wa Nuuh ambayo yalididimia kwenye udongo baada ya mafuriko. Hatimaye akayatafuta na kuyachimbua ambapo akawa ameyatawanya.

Masanamu haya yaliyokuwa yamerithiwa kutoka kwa watu wa Nuuh ndio yalikuwa masanamu makubwa. Vinginevyo kulikuwepo masanamu mengine mengi. Pambezoni na Ka´bah kulikuwa masanamu 360. al-Laat, al-´Uzzaa, Manaat mwengine wa tatu ndio yalikuwa masanamu yao makubwa[1].

[1] Tazama ”as-Swahiyh” al-Bukhaariy (06/73).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 14
  • Imechapishwa: 08/10/2016