07. Mtume wa mwisho ni Muhammad (صَلَّى اللّٰهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)

Mtume wa mwisho ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na yeye ndiye alivunja picha za watu hawa wema.

MAELEZO

Hali ya waarabu ya kidini kabla ya kutumwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa ni kuabudu mizimu. Ndipo Allaah akamtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa dini ya Ibraahiym ambayo ni kumpwekesha Allaah pekee. Alibaki Makkah akiwalingania katika Tawhiyd na akiwakemea kuyaabudu masanamu kwa miaka kumi na tatu. Wakamuitikia na kujisalimisha pamoja naye Makkah wale Allaah aliotaka kuwaongoza katika Maswahabah. Halafu Allaah akawapa ruhusa ya kuhajiri kwenda Uhabeshi na baadaye wakahamia al-Madiynah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yeye akahajiri kwenda al-Madiynah na wakakusanyika pambezoni naye Muhaajiruun na Answaar na wakawa ni majeshi wa Tawhiyd ambapo walikuwa wakiwapiga vita washirikina. Ilipofika mwaka wa nane wakaenda kuufungua mji wa Makkah ambapo Makkah ikawa chini ya uongozi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hapo ndipo alipoyavunja masanamu haya yaliyoko pambezoni mwa Ka´bah na zikaondoshwa picha zilizoko ndani ya Ka´bah. Akawatuma baadhi ya Maswahabah kuyaendea masanamu al-Laat, al-´Uzzaa na Manaat yaliyoko pambezoni mwa Makkah kuyavunja kukiwemo picha za watu wema hawa katika watu wa Nuuh. Hapo ndipo Tawhiyd ikaenea na shirki kutokomezwa – na himdi zote ni za Allaah. Hii ndio maana ya maneno ya Shaykh (Rahimahu Allaah):

“… alivunja picha za watu hawa wema.”

Hapa ilikuwa siku ile ya kufunguliwa Makkah. Allaah aliisafisha sehemu Yake takatifu kutokamana na masanamu haya na Tawhiyd ikaanza kupanuka tangu kutumilizwa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kipindi cha makhaliyfah waongofu na karne bora zote zilikuwa hazina shirki. Zilipoisha karne bora ndipo Taswawwuf na madhehebu ya Shiy´ah yakaenea. Hapo ndipo shirki ikajitokeza katika Ummah kwa kuyaabudu makaburi na kuwatukuza mawalii na waja wema mpaka hii leo. Shirki hii ipo katika Umamah. Lakini hata hivyo Allaah (Jalla wa ´Alaa) huteua walinganizi wakweli wenye kuwasimamishia hoja waja Wake na Allaah huwaongoza kupitia wao wale ambao Allaah anawatakia uongofu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 15
  • Imechapishwa: 08/10/2016