Wa kwanza wao ni Nuuh (´alayhis-Salaam).

MAELEZO

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ

“Hakika Tumekufunulia Wahy kama Tulivyomfunulia Wahy Nuuh na Mitume baada yake.” (04:163)

Aayah hii inafahamisha kuwa Mtume wa kwanza ni Nuuh (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nuuh ndio Mtume wa kwanza baada ya kujitokeza kwa shirki katika ardhi. Walifuatia Mitume wengine juu ya mfumo huu wa kiungu. Wa mwisho wao ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ndiye wa mwisho wao na wala hakuna Nabii mwingine baada yake mpaka pale Qiyaamah kitaposimama. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.” (33:40)

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi ndiye Nabii wa mwisho. Hakuna Nabii mwingine baada yangu.” at-Tirmidhiy (2219), Abu Daawuud (4252) na Ahmad (05/278).

Yeye ndio Mtume na Nabii wa mwisho (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kila Mtume ni Nabii vilevile. Allaah hatotuma baada yake si Nabii wala Mtume mwingine.

Kwa hiyo yule atayeitakidi kwamba Allaah atatuma baada yake Mtume au Nabii ni kafiri. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kutajitokeza baada yangu waongo thelathini. Kila mmoja katika wao anadai kuwa ni Nabii ilihali mimi ndiye Nabii wa mwisho na wala hakuna Nabii mwingine baada yangu.” at-Tirmidhiy (2219), Abu Daawuud (4252), Ibn Maajah (3952) na Ahmad (05/278).

Yule asiyeitakidi kuwa utume umemalizika kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akajuzisha kutumwa baada yake Nabii mwingine amemkufuru Allaah (´Azza wa Jall). Amemkadhibisha Allaah, Mtume Wake na maafikiano ya waislamu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 13
  • Imechapishwa: 08/10/2016