Abul-Hasan al-Ma´ribiy amesema:

“Kama unakusudia suala la maelezo ya mtu mmoja (خبر الآحاد), mimi ndiye nimepatia na sio Shaykh Rabiy´.”

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanajengea hoja kwa maelezo ya mpokezi mmoja. Maelezo ya mtu mmoja hoja ya lazima kutendewa kazi kwa yule yaliyemfikia. Maelezo kama hayo yanapelekea katika elimu na ulazima wa kuitendea kazi, kama inavyotambulika kwa jopo kubwa la wanazuoni.

Nakumbuka kuwa mwaka wa 1376 nilinunua kitabu “al-Umm” cha ash-Shaafi´iy na maelezo yake ya chini katika ile juzu ya mwisho “Ikhtilaaf-ul-Hadiyth”. Nikamsomea nacho Shaykh Haafidhw al-Hakamiy. Nikasoma “Ikhtilaaf-ul-Hadiyth” kipindi hicho na nikajifunza masuala hayo na pengine kipindi hicho ulikuwa hata bado kuzaliwa. Mfano wa yaliyosemwa na ash-Shaafi´iy mwanzoni mwa kitabu hicho:

“Iwapo mtu atauliza dalili iko wapi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba maelezo ya mtu mmoja yanatakiwa kukubaliwa, ataambiwa kuwa watu mwanzoni walikuwa wakiswali kwa kuelekea Yerusalemu. Kisha baadaye Allaah akawaamrisha kuelekea msikiti Mtakatifu. Alikuja mtu mmoja kutoka katika watu wa Qubaa´ akawakuta wamesimama wanaswali ambapo akawaelekeza kuwa Allaah amemfunulia Mtume Wake ya kwamba Qiblah kimegeuzwa kutoka Yeruslemu kuelekea msikiti Mtakatifu. Hivyo wakageuka wakiwa ndani ya swalah.

Dalili nyingine ni kuwa Abu Twalhah na wengine walikuwa wamekaa wakinywa pombe ambapo akaja mtu na kuwaeleza kuwa pombe imeharamishwa. Hivyo wakavunja mitungi yao ya vinywaji. Hapana shaka kuwa hawawezi kufanya kitu kama hicho pasi na kumweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Tukio hilo linafanana na maelezo ya mtu ambaye wanaona kuwa ni mkweli lakini ambaye maneno yake hawatakiwi kuyakubali kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaambia: “Mlikuwa mmelekea Qiblah. Hamkuwa mnatakiwa kugeuka mpaka mimi, au kikosi cha watu au idadi ya watu kadhaa wakuelezeni” na kwamba hoja inasimama juu yao kwa kiasi cha idadi ya watu mfano wake na si venginevyo.”[1]

Nimekueleza haya ili kukuonyesha kuwa umenifanyia utovu wa nidhamu wakati unaposema kuwa khbari zangu zote nazitoa kwa Shaykh Rabiy´. Kadhalika umefanya utovu wa adabu kwa Shaykh Rabiy´ wakati ulipomshambulia na kusema:

“Maelfu ya wanafunzi hawakubaliani na chochote alichoandika Shaykh Rabiy´ au alichosema.”

Hakuna ambaye amesema kuwa maelezo ya mpokezi mmoja hayapelekei katika elimu wala kuwajibisha kitendo isipokuwa Mu´tazilah na wanafalsafa wa Ashaa´irah. Baadhi yao wanasema kuwa maelezo ya mtu mpokezi mmoja hayakubaliwi katika mambo yanayohusu ´Aqiydah. Hivo ndivo anavosema al-Ghazaaliy wa sasa na baadhi ya al-Ikhwaan al-Muslimuun. Ibn Qudaamah amesema:

“Kiakili inafaa kumwabudu Allaah kwa maelezo ya mpokezi mmoja, tofauti na kundi la watu wanavosema. Hiyo ina maana kwamba kuna uwezekano Allaah (Ta´ala) akawawajibishia watu kumwabudu kwa maelezo ya mpokezi mmoja na akawaambia: “Niabuduni kwa mujibu wa yale yanayokufikieni kutoka Kwangu na Mtume Wangu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia maelezo ya mpokezi mmoja.” Haya ndio maoni ya kikosi kikubwa cha wanazuoni, maimamu wanne na Fuqahaa´ wengine na wanazuoni wengine wa misingi. al-Jubbaaiy na wanafalsafa wengine wanaonelea kinyume.”[2]

al-Jubbaaiy ni mmoja katika viongozi wa Mu´tazilah. Nyinyi mnamfuata al-Jubbaaiy na mmeacha kikosi kikubwa cha Muhaddithuun na Fuqahaa´ wakiwemo wale maimamu wanne. Hili linafahamisha waziwazi namna ambavyo umeshikilia Bid´ah; Bid´ah za Mu´tazilah ambao wanaona kuwa maelezo ya mpokezi mmoja hayapelekei katika elimu.

Maelezo ya mpokezi mmoja yanawajibisha elimu na kitendo. Si kwamba inafaa kuyakubali peke yake; bali ni lazima. Tunapojiliwa na maelezo ya mpokezi mmoja ya kwamba ni lazima kwa ambaye amegusa tupu yake kutawadha, kama inavosema Hadiyth ya Busrah[3], basi italazimika kuisadikisha na kuitendea kazi.

[1] Ikhtilaaf-ul-Hadiyth, uk. 476.

[2] Rawdhwat-un-Naadhwir (2/112).

[3] Busrah bint Swafwaan amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Yule mwenye kugusa dhakari yake basi atawadhe.” (Abu Daawuud (181) na at-Tirmidhiy (82). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud (175))

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tanbiyh al-Wafiy ´alaa Mukhaalafaat Abiyl-Hasan al-Ma’ribiy, uk. 304-307
  • Imechapishwa: 03/12/2022