Urefu wake ni mwezi, upana wake ni mwezi, pembe zake mbili ziko sawa, vikombe idadi yake ni sawa na nyota mbinguni, maji yake ni meupe zaidi kuliko maziwa, matamu zaidi kuliko asali na yenye harufu nzuri zaidi kuliko harufu ya miski. Ina mifereji inayovutwa kutoka Peponi; moja ni ya dhahabu na nyingine ni ya fedha. Itaendewa na waumini katika Ummah wa Muhammad. Atakayekunywa humo mara moja basi hatohisi kiu kamwe. Yote haya yamethibiti katika “as-Swahiyh” mbili au moja wapo[1]. Hivi sasa ipo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi, naapa kwa Allaah, ninaangalia Hodhi hivi sasa.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy.

Yanachukuliwa maji hayo kutoka katika al-Kawthar. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Amenipa al-Kawthar. Ni mto Peponi unaomimina maji ndani ya Hodhi.”[3]

Ameipokea Ahmad. Ibn Kathiyr amesema:

“Cheni ya wapokezi na matini yake ni nzuri.”

Kila Mtume anayo hodhi. Lakini hodhi yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio kubwa zaidi, tukufu zaidi na itayoendewa na watu wengi zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika kila Mtume anayo hodhi. Hakika watajifakharisha ni nani kati yao ambaye ataendewa na watu wengi. Hakika mimi nataraji ndio ambaye nitajiliwa na watu wengi.”

Ameipokea at-Tirmidhiy ambaye amesema:

“Geni.”

Ameyapokea hayo vilevile Ibn Abiyd-Dunyaa na Ibn Maajah kupitia kwa Abu Sa´iyd. Ndani yake kuna unyonge. Lakini baadhi yao wameisahihisha kutokana na wingi wa njia zake[4].

[1] al-Bukhaariy (6579) na Muslim (2292, 27).

[2] al-Bukhaariy (6590).

[3] al-Bidaaayh wan-Nihaayah (02/244). Katika cheni ya wapokezi yuko Ibn Lahiy´ah ambaye ni mnyonge.

[4] at-Tirmidhiy (2443).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 124-125
  • Imechapishwa: 04/12/2022