05. Mnasemaje kuhusu rehema, kushuka kwenye mbingu ya dunia na mfano wa hayo?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 5: Mnasemaje kuhusu rehema, kushuka kwenye mbingu ya dunia na mfano wa hayo?

Jibu: Tunaamini na kuthibitisha yale yote ambayo Allaah amejisifu Mwenyewe kwa huruma, kuridhia, kushuka na kuja. Kadhalika kwa yale yote ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemsifu nayo. Hili linatakiwa kufanywa kwa njia isiyofananishwa na kiumbe yeyote, kwa sababu Hakuna chochote kinachofanana Naye.

Kama jinsi Allaah ana dhati isiyofanana na dhati nyinginezo, kadhalika ana sifa zisizofanana na sifa nyinginezo.

Hili linathibitishwa na yale mapambanuzi makubwa katika Qur-aan na Sunnah ambapo sifa zimethibitishwa na ambapo Allaah amesifiwa nazo. Humo kadhalika amebainisha kutakasika na anaolingana Nao, wenza na washirika.

MAELEZO

Allaah amejisifu Mwenyewe kwa huruma na Yeye mwenyewe akajiita kuwa ni ar-Rahmaan (Mwingi wa huruma) na ar-Rahiym (Mwenye kurehemu). Ameeleza kuwa ana huruma mia na kwamba ameteremsha rehema moja ambayo ndio watu huhurumiana na mnyama anahakikisha hamkanyagi mtoto wake. Rehema zengine tisini na tisa zimebaki Kwake; atawahurumia kwazo waja Wake waumini siku ya Qiyaamah.

Haijuzu kupindisha sifa ya huruma, kama wanavofanya Ashaa´irah. Bali tunaamini kuwa sifa za Allaah hazifanani na sifa za viumbe.

Vilevile tunaamini kuwa Allaah (´Azza wa Jall) hushuka katika mbingu ya chini ya dunia katika theluthi ya mwisho ya usiku na husema mpaka alfajiri ikaingia:

“Kuna mwenye kuomba nimpe? Kuna mwenye kuomba nimuitikie? Kuna mwenye kuomba msamaha nimsamehe?”[1]

Tunaamini vilevile kwamba Allaah hushuka katika mbingu ya dunia mchana wa siku ya ´Arafah.

Tunaposema kuwa Allaah anashuka katika mbingu ya dunia tunamaanisha ushukaji unaolingana na utukufu Wake. Haijuzu kuuliza kama huiacha ´Arshi au haiachi. Hiki ni kitu kinachoulizwa katika sifa za viumbe. Yeye amejisifu Mwenyewe kwa kusema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[2]

Kama ambavo dhati ya Allaah haifanani na dhati za viumbe ndivo ambavo sifa Zake hazifanani na sifa za viumbe. Maneno ya mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah):

“Hili linathibitishwa na yale mapambanuzi makubwa katika Qur-aan na Sunnah ambapo sifa zimethibitishwa na ambapo Allaah amesifiwa nazo. Humo kadhalika amebainisha kutakasika na anaolingana Nao, wenza na washirika.”

Hiyo ina maana kwamba Allaah (´Azza wa Jall) ameitakasa nafsi Yake Mwenyewe kutokamana na wenye kulingana Naye na akasema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”

Vivyo hivyo hana (Subhaanah) washirika. Kadhalika hana wenza:

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

”Wala hakuna yeyote anayefanana na kulingana Naye.”[3]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameeleza kuwa hana washirika katika ufalme Wake:

ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ

“Huyo basi ndiye Allaah Mola wenu, ufalme ni Wake pekee. Na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende.”[4]

Amekhabarisha kwamba hawamiliki kijiwavu cha kokwa ya tende.

Yote haya yanathibitisha sifa za Allaah (´Azza wa Jall), yanamtakasa kutokamana na sifa za viumbe na yanampwekesha kwa sifa za kiungu ambazo hashirikiani ndani yake na yeyote.

[1] Muslim (758).

[2] 42:11

[3] 112:04

[4] 35:13

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 27/09/2021