27. Matunda ya elimu yenye manufaa na elimu isiyokuwa na manufaa

Msingi wa elimu ni utambuzi wa kumjua Allaah ambao unapelekea kumkhofu, kumpenda, kumkurubia, kuliwazika Naye na kuwa na shauku juu Yake. Kisha baada ya hapo kunafuatia utambuzi juu ya hukumu za Allaah na yale yote katika maneno, vitendo, hali na i´tiqaad Anazozipenda na Kuziridhia. Yule ambaye atakuwa na elimu hizi mbili basi elimu yake itakuwa yenye manufaa. Atapata elimu yenye manufaa, moyo wenye kunyenyekea, nafsi yenye kukinai na du´aa yenye kuitikiwa. Na yule mwenye kupitwa na elimu hii yenye manufaa basi ataingia katika yale mambo manne ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliomba kukingwa nayo. Elimu kama hiyo itakuwa ni maangamivu na hoja dhidi yake. Kwa sababu moyo wake haukunyenyekea kwa Mola Wake, nafsi yake haikushiba na dunia, bali imezidi kuwa na tamaa, na du´aa yake si yenye kuitikiwa kwa sababu ya kutotekeleza kwake maamrisho ya Mola Wake na kutojiepusha kwake na yanayomkasirisha na kuyachukia. Hapa ni pale ambapo ikiwa katika elimu yake kuna uwezekano wa kunufaika nayo kwa maana kwamba inatokana na Qur-aan na Sunnah. Ikiwa inatokana na yasiyokuwa hayo, basi si yenye manufaa yenyewe kama yenyewe na wala haiyumkiniki kunufaika kwayo. Bali madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake.

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 78-79
  • Imechapishwa: 28/09/2021