Alama ya elimu hii isiyokuwa na manufaa ni kumfanya mwenye nayo kuwa na jeuri, kujikwaza na kiburi. Anakuwa mwenye kutafuta ukuu na vyeo duniani. Anakuwa mwenye kutaka kushindana na wanazuoni, kuvutana na wapumbavu na kuyafanya macho ya watu kumgeukia yeye. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Usijifunze elimu kwa ajili ya kujifakharisha kwa wanazuoni, kugombana na wapumbavu wala kwa ajili ya kuingia katika vikao vizuri. Yule mwenye kufanya hivo basi ajihadhari na Moto ajihadhari na Moto.”[1]

Huenda wakadai baadhi ya wale wenye elimu hii utambuzi wa kumjua Allaah, kupambana kuitafuta elimu hiyo na kuyapa nyongo mengine yote. Hata hivyo lengo lao pekee ni kutafuta vyeo kwenye mioyo ya watu, kukiwemo wafalme, kuwajengea dhana nzuri na wingi wa wafuasi ambapo wanaweza kuwa juu ya watu wengine. Alama ya hilo ni kudai madai ya uwalii, kama walivokuwa wanadai watu wa Kitabu, Qaraamitwah, Baatwiniyyah na mfano wao. Haya ni tofauti kabisa na yale waliyokuwemo Salaf ambapo walikuwa wakizidharau nafsi zao kwa njia zote. ´Amr amesema:

”Ambaye atasema kuwa yeye ni mwanachuoni basi ni mjinga. Ambaye atasema kuwa yeye ni muumini basi ni kafiri. Ambaye atasema kuwa yuko Peponi basi yuko Motoni.”

[1]Ibn Maajah (254), Ibn Hibbaan (290), al-Aajurriy katika ”Akhlaaq-ul-´Ulamaa’”, uk. 84-85) na al-Haakim (1/86). Swahiyh kupitia zengine kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (107).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 79-80
  • Imechapishwa: 28/09/2021