05. Mageuzi na maporomoko ya ardhi

Kuhusu adhabu ni zenye kutofautiana:

1- Za kidunia. Adhabu za kidunia zimegawanyika aina mbili:

A- Zilizowekwa katika Shari´ah kama mfano wa kuuliwa baada ya kunywa kwa mara ya nne, jambo ambalo lina maneno yanayotambulika.

B- Adhabu za kilimwengu kama mfano wa kugeuzwa ngedere na nguruwe na maporomoko ya ardhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watakuweko watu katika Ummah wangu ambao watakunywa pombe na ala za muziki zitapigwa juu ya vichwa vyao. Allaah atawadidimiza chini ya ardhi na atawageuza ngedere na nguruwe.”[1]

Miongoni mwa adhabu zipo ambazo ni ndani ya kaburi, tutalitaja huko mbele. Mujaahid amesema:

“Hakuna yeyote anayekufa ilihali ni mzinzi, mwizi au chapombe, isipokuwa Allaah atamwekea ndani ya kaburi lake nyoka wawili wenye pembe wataokuwa wanamuuma hadi siku ya Qiyaamah.”

Sahl bin al-Anbaariy amesema:

“Nilimwendea bwana mmoja ambaye alikuwa anataka kukata roho. Wakati nilipokuwa kwake akapiga makelele na kushika magoti yangu. Akaniogopesha. Nikamwambia: “Una nini wewe?” Akasema: “Kule kuna muhabeshi wa bluu. Macho yake ni kama mapipa. Amenikamata na kunambia: “Mida ya adhuhuri utaenda Motoni.” Baada ya hapo nikauliza ni kipi bwana huyo alikuwa anafanya. Nikapata khabari kwamba alikuwa ni mnywaji mvinyo.”[2]

[1] Ibn Maajah (4020) na Ibn Hibbaan (6758).

[2] Ibn Abiyd-Dunyaa katika ”Kitaab-ul-Muhtadhwariyn”, uk. 164-165

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ul-Khamr, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 25/07/2020