04. Kunywa pombe kunafanya swalah na tawbah kutokukubaliwa

3- Kunywa pombe kunapelekea kutokukubaliwa swalah na tawbah

´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kunywa pombe na akalewa, basi hazitokubaliwa kwake swalah asubuhi arobaini. Akifa, basi ataingia Motoni, na akitubu, basi Allaah atamsamehe.”[1]

Kwa an-Nasaa´iy imekuja:

“Yule mwenye kunywa pombe na akalewa, basi Allaah hatomkubalia tawbah yake asubuhi arobaini.”[2]

Katika “al-Musnad” ya Ibn Wahb imekuja:

“Yule mwenye kunywa pombe na akalewa, basi Allaah atamkasirikia siku arobaini. Na akilewa mara ya nne, basi Allaah hatomridhia mpaka pale atapokutana Naye.”

at-Tirmidhiy amepokea:

“Na akilewa mara ya nne na akatubu, basi Allaah hatomsamehe. Badala yake atamnywesha jasho la wakazi wa Motoni.”[3]

Kama Hadiyth zitasihi basi zinalenga kwamba chapombe huyo baada ya hapo hakuongozwa katika tawbah ya kweli. Hivyo Hadiyth zitakuwa zimekuja kwa lengo la matishio na makemeo. Abu Daawuud amesimulia kupitia kwa Ibn ´Abbaas:

“Yule mwenye kunywa pombe basi anakuwa mchafu na swalah zake zinakuwa chafu kwa muda wa siku arobaini.”[4]

Swalah hazikubaliwi kwa muda wa siku arobaini kwa sababu ya kulewa. Pindi kunapokosekana kilevi basi inakuwa:

“Swalah zake hazikubaliwi kwa muda wa wiki.”

Namna hii ndivo ilivyopokelewa kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr na pia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ulevi usingekuwa na baya jingine zaidi ya kukosa kumwomba Mwingi wa rehema basi ingetosha kukaripiwa kwake.

[1] Ibn Maajah (3377) na Ibn Hibbaan (5357).

[2] an-Nasaa’iy (5670).

[3] at-Tirmidhiy (1862).

[4] Abu Daawuud (3680).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ul-Khamr, uk. 13-14
  • Imechapishwa: 25/07/2020