5 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Yeyote atakayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia… ”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth hii ni dalili juu ya ubora wa kusimama Ramadhaan na kwamba ni miongoni mwa sababu za kusamehewa madhambi. Yule ambaye ataswali Tarawiyh, kama inavotakikana, basi amesimama Ramadhaan. Msamaha umeshurutishwa kwa maneno yake:

“… kwa imani na kwa matarajio… “

Maana ya:

“… kwa imani… “

ni kwamba katika hali ya kusimama kwake awe ni mwenye kumwamini Allaah (Ta´ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na pia mwenye kusadikisha ahadi ya Allaah, ubora wa kisimamo na ukubwa malipo yake mbele ya Allaah (Ta´ala).

Maana ya:

“… kwa matarajio… “

ni kwamba awe mwenye kutarajia malipo mbele ya Allaah (Ta´ala). Kwa msemo mwingine asiwe na makusudio mengine ya kujionyesha na mengineyo.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikokoteza zaidi juu ya kusimama Ramadhaan pasi na kuwaamrisha kisha akisema:

“Yeyote atakayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Ni lazima kwa muislamu apupie kuswali Tarawiyh pamoja na imamu na wala asizembee katika chochote katika hayo. Asiondoke kabla ya imamu wake ijapo atazidisha juu ya Rak´ah kumi na moja au Rak´ah kumi na tatu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yulle atakayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza, basi anaandikiwa kusimama usiku mzima.”[2]

Inahusiana na nyusiku yenye kuhesabika ambayo anayatumia vizuri mwenye akili kabla ya kupita kwake.

Abu Daawuud amesema:

“Aliambiwa Ahmad na mimi nikisikia: “Je, kicheleweshwe kisimamo?” – bi maana Tarawiyh mpaka mwishoni mwa usiku?” Akasema: “Hapana. Sunnah ya waislamu ni yenye kupendeza zaidi kwangu.”[3]

Mtu akitaka kuswali kile kiasi alichowezeshwa wakati wa mwisho wa usiku, basi asiswali Witr mwishoni mwa swalah yake kwa mara nyingine. Bali inamtosha ile Witr aliyoswali pamoja na imamu wake katika swalah ya Tarawiyh mwanzoni mwa usiku. Twalq bin ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna Witr mbili katika usiku mmoja.”[4]

Kuhusu Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ifanyeni swalah yenu ya mwisho ni Witr.”[5]

inachukuliwa kwa njia ya yule aliyeswali mwishoni mwa usiku na hakuswali Witr mwanzoni mwake. Amri ni kwa njia ya mapendekezo na si kwa njia ya ulazima. Kwa hivyo si lazima kumalizia swalah mwishoni mwa usiku kwa Witr. Dalili ya hilo ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipatapo kuswali baada ya Witr mwishoni mwa usiku[6].

Atakapotoa salamu mswaliji baada ya Witr atasema:

سبحان الملك القدوس, سبحان الملك القدوس, سبحان الملك القدوس

“Ametakasika Mfalme, Mtakatifu. Ametakasika Mfalme, Mtakatifu. Ametakasika Mfalme, Mtakatifu.”

Ataivuta na kuinyanyua sauti yake juu ile mara ya tatu. Hayo yamethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[7].

Ee Allaah! Ziamshe nyoyo zetu kutokana na usingizi wa matumaini, tukumbushe kukaribia kuondoka na kumalizika kwa kipindi cha kuishi, zithibitishe nyoyo zetu juu ya imani, tuwafikishe katika matendo mema na tusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (2009) na Muslim (759).

[2] Abu Daawuud (1375), at-Tirmidhiy (806), an-Nasaa´iy (03/203) na Ibn Maajah (01/420). at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

[3] Masaail Imaam Ahmad, uk. 62 ya Abu Abu Daawuud.

[4] Abu Daawuud (1439), at-Tirmidhiy (470), an-Nasaa´Iy (03/229) na Ahmad (26/222). at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth hii ni nzuri na ngeni.”

Ni nzuri kwa mujibu wa Haafidhw Ibn Hajar. Tazama ”Fath-ul-Baariy” (02/481).

[5] al-Bukhaariy (998) na Muslim (751) na (151).

[6] Ibn Khuzaymah na wengineo kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Swahiyh Ibn Khuzaymah (02/159).

[7] Abu Daawuud (1430), an-Nasaa´iy (03/244), Ibn Maajah (1171) na Ahmad (35/80). Ni Hadiyth Swahiyh. Imekuja kwa ad-Daaraqutwniy katika ”Sunan” yake (02/31) nyongeza inayosema:

رب الملائكة والروح

”Mola wa Malaika na Roho.”

Nyongezi hii haikuhifadhiwa. Tazama ”Takhriyj Ahaadiyth-idh-Dhikhr wad-Du´aa´ lil-Qahtwaaniy” (01/361) ya Shaykh Yaasir bin Fathiy al-Miswriy.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 18/04/2022