6 – Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Isomeni Qur-aan kwani itakuja siku ya Qiyaamah hali ya kuwa ni yenye kuwaombea watu wake.”[1]

Ameipokea Muslim.

Katika Hadiyth kuna ubora wa usomaji Qur-aan, ukubwa wa thawabu na kwamba itakuja siku ya Qiyaamah hali ya kuwa ni yenye kuwaombea watu wake kuingia Peponi.

an-Nawwaas bin Sam´aan (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Italetwa Qur-aan siku ya Qiyaamah na watu wake waliokuwa wakiifanyia kazi ikitanguliwa na Suurah “al-Baqarah” na “Aal ´Imraan”. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akazipigia mifano mitatu ambayo sintoisahau baada yake. Akasema: “Kana kwamba viwili hivyo ni mawingu mawili au kanopi mbili nyeusi ambazo kati yazo kuna nuru au kana kwamba viwili hivyo ni njia mbili za kundi la ndege watawatetea watu wao.”[2]

Kwa hivyo mfungaji anatakiwa kusoma Qur-aan kwa wingi katika masiku haya yaliyobarikiwa na nyusiku tukufu. Kusoma Qur-aan kwa wingi ndani ya Ramadhaan kuna sifa ya kipekee isiyopatikana katika miezi mingine ili aweze kuchuma tukufu wa wakati katika mwezi huu ambao Qur-aan imeteremshwa ndani yake. Kuna sifa ya kipekee ya kusoma Qur-aan ndani ya nyusiku za Ramadhaan. Usiku kazi zinakatika, msukumo unakusanyika na inaathiri moyo na ulimi zaidi kwa kuzingatia. Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada. Haafidhw Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hakika si venginevo kumepokelewa makatazo ya kusoma Qur-aan yote ndani ya siku tatu kwa njia ya mtu kudumu katika jambo hilo. Kuhusu vipindi bora, kama mfano wa nyusiku za Ramadhaan na khaswa nyusiku ambazo kunatafutwa ndani yake usiku wenye cheo au katika maeneo matuufu, kama mfano wa Makkah kwa aliyeingia ndani yake katika wasiokuwa wakazi wake, inapendeza kusoma Qur-aan kwa wingi kwa ajili ya kuchuma ubora wa vipindi na maeneo. Haya ndio maoni ya Ahmad, Ishaaq na maimamu wengineo. Matendo ya wengine yanafahamisha jambo hilo kama tulivyotangulia kuzitaja.”[3]

Ni lazima kwa msomaji kujipamba na adabu za kisomo ambazo anatakiwa kujipamba nazo ikiwa ni pamoja na:

1 – Kumtakasia nia Allaah (Ta´ala).

2 – Kusoma akiwa na twahara.

3 – Kutumia Siwaak.

Kufanya mambo hayo ni katika kuyaadhimisha maneno ya Allaah (´Azza wa Jall).

4 – Ni lazima kwake kusoma kwa kutamka. Ambaye atatosha kusoma kwa kuangalia peke yake hazingatiwi kasoma na hapati thawabu za kisomo[4].

5 – Ni lazima kwake kuyazingatia yale anayoyasoma. Kwa sababu hayo ni miongoni mwa malengo yanayotakiwa[5].

6 – Miongoni mwa adabu za kisomo ni msomaji asujudu pale atapoipitia Aayah ya kisomo ilihali ametawadha pasi na kujali ni wakati gani.

7 – Asisome kwa sauti kwa njia ya kwamba akawakera walioko pambizoni mwake. Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliikaa I´tikaaf msikitini. Akawasikia wakisoma kwa sauti za juu akiwa kwenye hema lake akafunua pazia na kusema: “Zindukeni! Nyote ni wenye kumng´oneza Mola Wenu. Kwa hivyo baadhi wasiwaudhi wengine na baadhi yenu wasiwanyanyulie wengine kisomo” au alisema “… katika swalah.”[6]

Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Ee Allaah! Ifanye Qur-aan tukufu kuwa ni mlezi wa nyoyo zetu, nuru ya vifua vyetu, kutuondolea huzuni zetu, kutuondolea hamu zetu na kutuongoza Kwako na kwenda katika Pepo yenye neema. Ee Allaah! Tukumbushe kutoka kwayo tuliyoyasahau, tufunze kwayo tusiyoyajua na tujaalie kuisoma kwa wingi kwa mujibu wa vile unavopenda na kuridhia. Tusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] Muslim (804).

[2] Muslim (805).

[3] Latwaaif-ul-Ma´aarif, uk. 201-202.

[4] Tamhiyd (11/46) ya Ibn ´Abdil-Barr na ”Fataawaa Ibn Baaz” (24/381).

[5] at-Tidhkaar fiy Fadhwl-il-Adhkaar, uk. 109 ya al-Qurtwubiy.

[6] Abu Daawuud (1332), an-Nasaa´iy katika ”al-Kabiyr” (07/288, 289) na Ahmad (18/392-393). al-Albaaniy amesema:

”Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.” Tazama ”as-Swahiyhah” (04/134).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 18/04/2022