04. Washirikina wa kale walikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na wakapinga Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukishahakikisha ya kwamba walikuwa wanakubali hili, lakini hili halikuwaingiza katika Tawhiyd ambayo aliwalingania kwayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na ukajua ya kwamba Tawhiyd waliyoipinga ni Tawhiyd-ul-´Ibaadah ambayo washirikina katika zama zetu wanaiita “al-I´itiqaad”, kama walivyokuwa wakimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) usiku na mchana. Halafu katika wao kulikuwa wanaowaomba Malaika kwa ajili ya wema wao na ukaribu wao kwa Allaah ili wawaombee, au wanamuomba mtu mwema, kama mfano wa Laat, au Mtume kama mfano wa ´Iysa – na ukajua ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kawapiga vita kwa ajili ya shirki hii na akawaita kumtakasia ´Ibaadah Allaah pekee. Kama Alivyosema (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

 “Na kwamba mahala pote pa kuswalia ni kwa ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (al-Jinn 72 : 18)

لَهُ دَعْوَةُ الْحَقِّ ۖ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَجِيبُونَ لَهُم بِشَيْءٍ

“Kwake ndiko kuna maombi yote ya haki. Na wale wanaoomba pasi Naye hawawaitikii kwa chochote.” (ar-Ra´d 13 : 14)

na umehakikisha ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita ili du´aa [maombi] yote yawe kwa Allaah, nadhiri zote awekewe Allaah, kuchinja kote kuwe kwa Allaah, kuomba uokozi kote kuwe kwa Allaah na aina nyenginezo zote za ´Ibaadah afanyiwe Allaah, na umejua kuwa kukubali kwao Tawhiydur-Rubuubiyyah hakukuwaingiza katika Uislamu na kwamba kuwakusudia kwao Malaika, au Mitume na mawalii hakuna jengine walichokuwa wanataka isipokuwa tu maombezi yao na kujikurubisha kwa Allaah kwa hilo, ndio yaliyofanya kuhalalika damu yao na mali zao, hapo ndipo utajua Tawhiyd waliyoilingania kwayo Mitume na washirikina wakakataa kuikubali.

Tawhiyd hii, ndio maana ya maneno yako: “Hapana mungu isipokuwa Allaah”. Kwa hakika mungu kwa mujibu wao ni yule ambaye anakusudiwa [anayeombwa] kwa ajili ya mambo haya1 , sawa ikiwa ni Malaika, Mtume, walii, mti, kaburi au jini. Hawamaanishi ya kwamba mungu ni yule mwenye kuumba, mwenye kuruzuku na mwenye kuyaendesha mambo. Kwa kuwa wao wanajua ya kwamba hayo ni ya Allaah pekee, kama tulivyotangulia kusema.

Mungu wanayemaanisha ni yule ambaye washirikina wa zama zetu wanamaanisha kwa kusema “bwana”. Akawajia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwalingania katika kalima ya Tawhiyd, nayo ni “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Na makusudio ya maneno haya ni maana yake na sio kuyatamka peke yake.

Makafiri wajinga walijua kuwa anachokusudia Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) kwa neno hili ni kumpwekesha Allaah (Ta´ala) kwa ´Ibaadah na kukanusha vyote vinavyoabudiwa badala Yake na kujiweka navyo mbali kabisa. Hakika wakati alipowaambia waseme “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”, walisema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya miungu wote kuwa ni mungu mmoja? Hakika hili ni jambo la ajabu mno.” (Swaad 38 : 05)

Ukishajua ya kwamba makafiri wajinga walijua hilo, jambo la kushangaza ni kwa yue anayedai Uislamu na yeye hajui maana ya neno hili jambo ambalo walikuwa wanalijua wajinga makafiri. Badala yake anafikiria ya kwamba maana yake ni kutamka herufi zake bila ya kuiamini moyoni kwa kitu katika maana yake. Mjuzi katika wao anafikiria ya kwamba maana yake ni kwamba hakuna mwenye kuumba, wala mwenye kuruzuku, wala mwenye kuyaendesha mambo isipokuwa Allaah. Hakuna kheri kwa mtu ikiwa wajinga makafiri wanajua zaidi yake maana ya “hapana mungu isipokuwa Allaah”.

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukishahakikisha yaliyotangulia tuliyotaja kwamba washirikina wanakubali ya kwamba Allaah ndiye Mwenye kuumba, Mwenye kuruzuku, Mwenye kuyaendesha mambo, kwamba Yeye ndiye Mwenye kuhuisha wafu, kwamba ndiye Mwenye kuteremsha mvua na kwamba Yeye juu ya kila jambo ni muweza katika yale anayoyaendesha (Subhaanahu wa Ta´ala). Lakini pamoja na haya walipinga Tawhiyd-ul-´Uluuhiyyah na kumtakasia Allaah ´ibaadah. Sambamba na hilo ni kwamba walikuwa wanaona kuwa hakuna ubaya wowote kuwategemea waja wema, kama mfano wa al-Laat, au kufungamana na Mitume, kama mfano wa ´Iysaa au wengineo katika mawe na miti kwa sababu ya kutafuta baraka na uombezi. Hivo ndivyo walivyofanya kwa al-´Uzzaa, Manaat, al-Laat, ´Iysaa na mama yake, Malaika na wengineo. Wao walikuwa wanaona kuwa mtu kufungamana na watu hawa, akaomba uombezi kutoka kwao, akawachinjia na kuwawekea nadhiri hakuna neno na haifai kukataza mambo hayo. Kwa ajili hiyo ndio maana walimkemea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu mambo hayo na wakati alipowaambia waseme “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah” wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu mno!”[1]

يَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ بَلْ جَاءَ بِالْحَقِّ وَصَدَّقَ الْمُرْسَلِينَ

”Wanasema: ”Je, sisi kweli tuache waabudiwa wetu kwa ajili ya mshairi mwendawazimu? Bali amekuja kwa haki na amewasadikisha Mitume.”[2]

Wao walikuwa hawampingi kuhusu kwamba Allaah ndiye Mola wao, Mwenye kuwaruzuku, Mwenye kuwateremshia mvua na Mwenye kuwaletea jua na mwezi. Wanayatambua mambo hayo. Lakini walimkemea pindi alipowalingania katika kumpwekesha Allaah, kumtakasia Yeye nia, kuacha kuweka nadhiri, kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah na mfano wa hayo katika yale waliyokuwa wakiyafanya. Walikuwa wanaona kuwa kuweka nadhiri na kumuomba asiyekuwa Allaah ni sawa na kwamba kufanya hivo ni kwa minajili ya kuelekea kwao na kujikurubisha kwao:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[3]

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie.”[4]

Sisi hatukusudii kuwa wanaumba, wanaruzuku na wanaendesha mambo. Walikuwa wanatambua kwamba yote haya yanaweza Allaah pekee. Lakini malengo yao walikuwa wanataka wawakurubishe kwa Allaah. Haya yaliyosemwa na washirikina wa kale na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawakemea kwayo ndio yaleyale yanayosemwa na hawa waliokuja nyuma. Washirikina waliokuja nyuma wanasema katika kufungamana kwao na wafu, Mitume na waja wema ya kwamba wanataka uombezi kutoka kwao kwa hoja eti wako na jaha. Matokeo yao wanawaabudu kwa sababu eti wawaombee kwa Allaah na wawanufaishe mbele ya Allaah. Haya yanayosemwa na watu hawa ndio yaleyale yaliyosemwa na wale wa zamani. Lakini washirikina wa zamani shirki yao ni khafifu kidogo. Kwa sababu washirikina wa kale walikuwa wakishirikisha kipindi cha raha na katika kipindi cha tabu wanamtakasia Allaah ´ibaadah. Ama washirikina hawa waliokuja nyuma shirki zao zinakuwa wakati wote wa raha na wa shida. Wanafanya hivo juu ya waja wema na wengineo.

[1] 38:05

[2] 37:36-37

[3] 10:18

[4] 39:03

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 14-16
  • Imechapishwa: 11/10/2021