05. Ni lazima kupambanua kati ya dini ya washirikina na dini ya waislamu

Ni wajibu kwako uweze kupambanua mambo juu ya jambo hili na ujue kuwa dini ya washirikina ni kinyume na dini ya waislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwalingania katika kumpwekesha Allaah. Allaah aliwatuma ili walinganie katika kumpwekesha Allaah, kumtii Allaah, kuacha kumshirikisha Allaah (Subhaanah) na awalinganie katika kuacha maasi. Wao walipokea ujumbe huu kwa upinzani, kufanya uadui, magomvi na wakapambana kwa ajili ya haya. Vita vya Badr, Uhud na al-Ahzaab zote zilikuwa kwa sababu ya kuitetea dini yao ya batili, kumtegemea kwao asiyekuwa Allaah na wakamshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Lakini Allaah akamsaidia Mtume Wake na akamnusuru dhidi yao mpaka akaweza kuukomboa mji wa Makkah na watu wakaingia katika dini ya Allaah makundi kwa makundi. Yote yanayohusiana na ulinganizi yanafahamisha maana hii na kwamba yule anayelinganiwa ikiwa anawategemea wafu, nyota na vyenginevyo ndiye ambaye anatakiwa kupewa kipaumbele katika kulinganiwa na kubainishiwa. Ama kitendo cha mtu kushirikisha katika utendakazi wa Allaah ni shirki iliyozidi ambayo ni mbaya zaidi kuliko ya wale wa kale. Mtu akidai kwamba Shaykh lake anaendesha ulimwengu na kwamba anayaendesha mambo, basi huyu shirki yake ni kubwa zaidi kuliko ya Abu Jahl na watu mfano wake.

Wale washirikina wa kale walitambua kumfanyia Allaah Tawhiyd inapokuja katika utendakazi wa Allaah; uumbaji, uruzukaji na kuyaendesha mambo. Sambamba na hilo wakamshirikisha Allaah katika ´ibaadah; khofu, kutaraji, swawm, uchinjaji, nadhiri na mfano wake. Kuhusu hawa washirikina waliokuja nyuma shirki yao inakuwa wakati wote wa raha na wa shida na vilevile inakuwa pamoja na waja wema na wengineo. Hivyo wakawa ni wenye shirki nyingi zaidi na mbaya zaidi kuliko wale washirikina wa zamani. Hayo ni kwa sababu ya kule kuchukulia kwao wepesi, ukaidi wao na kutokukubali nasaha. Sababu nyingine ni kwa kuwa wanashirikisha katika kipindi cha raha na shida.

Kwa ajili hiyo muumini anatakiwa kuzinduka juu ya jambo hili na atambue kuwa shirki ni kule kumtekelezea ´ibaadah, au baadhi yake, mwingine asiyekuwa Allaah. Ni mamoja kafiri huyo anaikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah au haikubali. Vovyote itavyokuwa hali yake ni kafiri midhali anamwabudu mwengine asiyekuwa Allaah, anamuomba uokozi mwingine asiyekuwa Allaah na anamuomba asiyekuwa Allaah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 11/10/2021