04. Ulazima wa kuwa na utambuzi juu ya Allaah na aina za elimu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la kwanza: Ujuzi. 

MAELEZO

Elimu – Makusudio ya elimu hapa ni elimu ya dini. Kwa sababu hii ndio ambayo ni lazima kuisoma. Masuala haya ni lazima kwa kila muislamu, mume kwa mke, muungwana kwa mtumwa, tajiri kwa masikini, mfalme kwa mmilikiwa, kujifunza nayo. Ni lazima kwa kila muislamu kujifunza masuala haya mane. Aina hii hapewi udhuru yeyote kutoyajua. Hii ndio ile elimu inayoitwa kuwa ni wajibu kwa kila muislamu. Nayo ni ile ambayo ni lazima kwa kila mmoja katika waislamu. Swalah tano kwa wanaume na kwa wanawake na swalah ya mkusanyiko misikitini kwa wanaume. Mambo haya ni lazima kwa kila mmoja katika waislamu kujifunza nayo. Kwa ajili hiyo amesema:

“Ni wajibu juu yetu.”

Hakusema kuwa ni wajibu kwa baadhi yetu. Amesema kuwa ni wajibu juu yetu akimaanisha sisi waislamu. Hii ni miongoni mwa elimu ambayo ni lazima kwa kila mmoja kujifunza nayo. Kwa sababu elimu imegawanyika aina mbili:

Aina ya kwanza: Ile elimu ambayo ni lazima kwa kila mmoja kujifunza nayo. Hapewi yeyote udhuru wa kutoijua. Ni ile ambayo dini haisimami isipokuwa kwayo. Kwa mfano nguzo tano za Uislamu ambazo ni shahaadah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba tukufu ya Allaah. Haijuzu kwa muislamu kutoyajua. Bali ni lazima kuyasoma. Kujifunza maana ya shahaadah inahusiana na kujifunza ´Aqiydah. Muislamu anatakiwa kujifunza ´Aqiydah ili aifanyie kazi na ajifunze yanayopingana nayo ili ajiepushe nayo. Haya ndio madhumuni ya shahaadah. Vivyo hivyo anatakiwa kujifunza nguzo za swalah, sharti za swalah, mambo ya wajibu ya swalah na mambo yaliyopendekezwa ya swalah. Anapaswa kujifunza kwa upambanuzi mambo haya. Si kuvurumisha swalah tu ilihali hajui hukumu za swalah. Ni vipi mtu atafanya kitendo ilihali hajui kitendo hichi anachokitekeleza? Ni vipi ataswali ilihali hajui hukumu zake? Kwa hiyo ni lazima ajifunze hukumu za swalah na mambo yanayoharibu swalah. Ni lazima ayasome mambo haya. Kadhalika ajifunze hukumu za zakaah, hukumu za swawm na hukumu za hajj. Akitaka kuhiji basi ni lazima kwake kujifunza hukumu za hajj na hukumu za ´umrah ili azitekeleze ´ibaadah hizi kwa njia iliyowekwa katika Shari´ah. Aina hii hapewi udhuru yeyote kutoijua. Hii ndio ile aina inayoitwa kuwa ni ya lazima kwa kila muislamu.

Aina ya pili: Ni ile elimu ni kile chenye kuzidi juu ya hapo katika hukumu za Kishari´ah ambazo watu wote wanazihitajia na pengine si kila mmoja anazihitajia. Kwa mfano hukumu za biashara, hukumu za miamala, hukumu za wakfu, hukumu za mirathi, wasia, hukumu za ndoa na jinai. Hukumu kama hizi ni lazima Ummah wazisome. Lakini si lazima kwa kila mmoja katika Ummah ajifunze nazo. Bali wanachuoni ambao malengo yatafikiwa kupitia wao wakijifunza nazo itatosha ili wasimamie haja za waislamu katika mambo ya uhakimu, kutoa fatwa, kusomesha na mengineyo. Hii ndio ile alimu inayoitwa faradhi yenye kutosheleza ambayo ikisimamiwa na wenye kutosheleza basi madhambi yanaporomoka kwa waliobaki. Watu wote wakiiacha wanapata dhambi. Ni lazima katika Ummah wawepo watu wataojifunza aina hii. Kwani wanaihitajia. Lakini haisemwi kwamba ni lazima kwa kila mmoja kuyasoma mambo haya. Kwa sababu huenda hilo lisimjie kila mmoja. Haya ni maalum kwa wale wenye uwezo katika Ummah. Jengine ni kwa sababu baadhi ya watu katika Ummah wakijifunza mambo haya basi watasimamia yale mambo ya wajibu. Hiyo ni tofauti na ile aina ya kwanza. Kila mmoja ni mwenye jukumu kwayo kwa nafsi yake. Kwa sababu matendo haya hayawezi kutendwa isipokuwa kwa elimu. Kwa ajili hiyo ndio maana Shaykh akasema:

“Ni wajibu juu yetu.”

Hakusema kuwa ni wajibu kwa waislamu au ni wajibu kwa baadhi yao. Bali amesema kuwa ni wajibu kwetu au kwa msemo mwingine kwa kila mmoja katika sisi. Inahusiana na ulazima wa kila mmoja kwa dhati yake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 13-19
  • Imechapishwa: 18/11/2020