Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Vilevile akufanye kuwa ni miongoni mwa wale wanapopewa basi hushukuru, wanapopewa mtihani basi husubiri na wanapotenda dhambi huomba msamaha. Hakika mambo haya matatu ndio ufunguo wa furaha.

MAELEZO

Alama za furaha ni kwamba mtu anapopata neema hushukuru, anapopatwa na mtihani husubiri na anapotenda dhambi huomba msamaha. Mtu hatoki nje ya hali hizi tatu. Upambanuzi wake ni ifuatavyo:

1 – Awe ndani ya neema na hivyo anapaswa kuishukuru. Kushukuru kunapatikana kwa mambo matatu; kwa ulimi, moyo na viungo vya mwili.

2 – Mtu awe amepewa mtihani katika nafsi yake kwa ugonjwa, umasikini, kufisha mtoto wake au mke wake. Anatakiwa awe mwenye kusubiri. Asikate tamaa na wala asikasirike. Msingi wa hilo ni yeye kuuzuia ulimi wake kutokana na kulalamika, azuie viungo vyake kutokana na yale yenye kumkasirisha Allaah na aizuie nafsi yake kutokana na kukata tamaa. Kwa maana nyingine asijipige mashavu na wala asipasue mfuko. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Umm Salamah wakati alipofariki Abu Salamah:

“Usiseme isipokuwa kheri. Kwani hakika Malaika wanaitikia “Aamiyn” kwa yale myasemayo.”[1]

3 – Mtu awe mtenda dhambi. Anapaswa kujikwamua kutokana na dhambi, ajutie yale yaliyotangulia, aazimie kutorudi na aombe msamaha. Aidha arudishe kile alichodhulumu kwa mwenye nacho.

Kwa hivyo mtu daima anakuwa katika neema na hivyo anashukuru, mtihani na hivyo anasubiri au dhambi na hivyo anaomba msamaha. Ikiwa mtu anamshukuru Allaah kutokana na neema, anasubiri juu ya mtihani na anatubu na kuomba msamaha pindi anapotenda dhambi. Mambo haya matatu ndio ufunguo wa furaha.

[1] Muslim (04/478).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 119-120
  • Imechapishwa: 03/03/2023