04. Elimu ambayo ni ujinga


Buraydah amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Baadhi ya ufaswaha ni uchawi na baadhi ya elimu ni ujinga.”

Swa´swa´h Swuhaan amesema kuhusu elimu ambayo ni ujinga:

“Ni kule mwanachuoni kujikakama juu ya elimu yake yale asiyoyajua, jambo ambalo humtia ujingani.”

Ameipokea Abu Daawuud[1].

Tafsiri nyingine ni kwamba ni ile elimu yenye kudhuru na hainufaishi ujinga. Kwa msemo mwingine ni bora kuwa mjinga kuliko kuijua elimu kama hiyo. Mambo yakishakuwa hivo kwamba ni bora kuijahili, basi ni ovu zaidi kuliko ujinga. Mfano wa elimu kama hiyo ni kama uchawi na nyenginezo ambazo zinadhuru katika ulimwengu au katika dini.

Kumepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) elimu nyingi zisizonufaisha. Zayd bin Aslam amesema:

“Kulisemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Ni mjuzi aliyoje fulani!” Akasema: “Juu ya nini?” Wakasema: “Nasaba za waarabu.” Ndipo akasema: “Ni elimu isiyonufaisha na ni ujinga usiyodhuru.”

Ameipokea Abu Daawuud katika “al-Maraasiyl”.

Ameipokea vilevile Abu Nu´aym katika “Riyaadh-ul-Muta´allimiyn” kupitia kwa Baqiyyah, kutoka kwa Ibn Jurayj, kutoka kwa ´Atwaa´, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Humo imekuja kwamba wamesema:

“Mjuzi wa watu juu ya nasaba za waarabu, mjuzi juu ya mashairi na mjuzi juu ya yale ambayo waarabu wametofautiana.” Amezidisha mwishoni mwa Hadiyth: “Elimu ni sampuli tatu, nyenginezo zote ni kitu chenye kuzidi: Aayah yenye maana ya wazi,Sunnah yenye kuendelea na faradhi adilifu.”[2]

Cheni ya wapokezi si yenye kusihi kwa sababu Baqiyyah amefanya tadliys kutoka kwa mtu asiyekuwa mwaminifu. Sehemu ya mwisho ya Hadiyth ameipokea Abu Daawuud na Ibn Maajah kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anhumaa), kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Elimu ni sampuli tatu, nyenginezo zote ni kitu chenye kuzidi: Aayah yenye maana ya wazi,Sunnah yenye kuendelea na faradhi adilifu.”[3]

Katika mlolongo wa wapokezi yuko ´Abdur-Rahmaan bin Ziyaad al-Ifriyqiy ambaye ana unyonge unaotambulika.

[1] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (5012).

[2]Ibn ´Abdil-Barr katika “al-Jaami´” (2/23).

[3] Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan Abiy Daawuud” (2885).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 39-42
  • Imechapishwa: 13/09/2021