03. Du´aa ya kuomba elimu yenye manufaa, du´aa dhidi ya elimu isiyokuwa na manufaa


Mfano wa elimu ambayo Allaah (Ta´ala) ameitaja katika mazingira ya kuisimanga ni pamoja na uchawi:

وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ۚ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا بِهِ أَنفُسَهُمْ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ وَلَوْ أَنَّهُمْ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَمَثُوبَةٌ مِّنْ عِندِ اللَّـهِ خَيْرٌ ۖ لَّوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ

”Wanajifunza yanayowadhuru na wala hayawanufaishi. Na kwa hakika walijua kuwa atakayechuma haya hatopata katika Aakhirah fungu lolote – na ni ubaya ulioje walichojiuzia nafsi zao endapo wangelikuwa wanajua.”[1]

Mfano mwingine ni:

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَرِحُوا بِمَا عِندَهُم مِّنَ الْعِلْمِ

“Basi walipowajia Rusuli wao kwa hoja bayana, walifurahia kwa kujivunia kwa yale waliyokuwa nayo katika elimu.”[2]

Vilevile amesema:

يَعْلَمُونَ ظَاهِرًا مِّنَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ عَنِ الْآخِرَةِ هُمْ غَافِلُونَ

“Wanajua ya juujuu katika mambo ya uhai wa dunia, lakini kuhusu Aakhirah wameghafilika [nayo].”[3]

Ndio maana Sunnah ikaja kugawanya kati ya elimu yenye manufaa na elimu isiyokuwa na manufaa. Sunnah pia imekokoteza watu waombe ulinzi dhidi ya elimu isiyokuwa na manufaa na wakati huohuo waombe elimu yenye manufaa. Zayd bin Arqam (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

اللَّهُمَّ إنِّي أَعُوذُ بكَ مِن عِلْمٍ لا يَنْفَعُ، وَمِنْ قَلْبٍ لا يَخْشَعُ، وَمِنْ نَفْسٍ لا تَشْبَعُ، وَمِنْ دَعْوَةٍ لا يُسْتَجَابُ لَهَا

“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na elimu isiyonufaisha, moyo usiyoogopa, nafsi isiyoshiba na du´aa isiyojibiwa.”[4]

Imepokelewa na Muslim, at-Tirmidhiy na an-Nasaa´iy kupitia njia nyingi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika baadhi ya mapokezi imekuja:

اللَّهُمَّ إنِّي أَعُوذُ بكَ مِن عِلْمٍ لا يَنْفَعُ، وَمِنْ قَلْبٍ لا يَخْشَعُ، وَمِنْ نَفْسٍ لا تَشْبَعُ، وَمِنْ ودعاءٍ لا يُسمعُ

“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na elimu isiyonufaisha, moyo usiyoogopa, nafsi isiyoshiba na du´aa isiyosikizwa.”[5]

Katika baadhi ya mapokezi imekuja:

اللَّهمَّ إني أعوذُ بك من علمٍ لا ينفعُ ، وقلبٍ لا يخشعُ ، ودعاءٍ لا يُسمعُ ، ونفسٍ لا تشبعُ ثم يقولُ : اللَّهمَّ إني أعوذُ بك من هؤلاءِ الأربعِ

“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na elimu isiyonufaisha, moyo usiyoogopa, du´aa isiyosikizwa na nafsi isiyoshiba na du´aa. Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba ulinzi dhidi ya mambo haya mane.”

Jaabir amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

اللَّهمَّ إنِّي أسأَلُكَ عِلمًا نافعًا و أَعُوذُ بكَ مِن عِلْمٍ لا يَنْفَعُ

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba elimu yenye manufaa na naomba kinga Kwako na elimu isiyonufaisha.”

Ameipokea an-Nasaa´iy.

Ibn Maajah amepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwombeni Allaah elimu yenye manufaa na takeni kinga kwa Allaah kutokamana na elimu isiyonufaisha.”

Abu Hurayrah amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

اللهم انفَعْنِي بما علَّمْتَني وعلِّمْنِي ما ينفَعُني وزِدْنِي علْمًا

“Ee Allaah! Ninufaishe kwa yale uliyonifunza, nifunze yatayoninufaisha na unizidishie elimu.”

Ameipokea at-Tirmidhiy[6].

Anas ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba:

اللهم انفَعْنِي بما علَّمْتَني وعلِّمْنِي ما ينفَعُني وارزقني علماً تنفعني به

“Ee Allaah! Ninufaishe kwa yale uliyonifunza, nifunze yatayoninufaisha na uniruzuku elimu itayoninufaisha.”[7]

Ameipokea an-Nasaa´iy.

Anas ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

“Ee Allaah! Hakika sisi tunakuomba imani daima; pengine imani ikawa si ya daima. Na nakuomba elimu yenye manufaa; pengine elimu isiwe yenye kunufaisha.”

Ameipokea Abu Nu´aym.

[1] 2:103

[2] 40:83

[3] 30:7

[4] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (123).

[5] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Jaami´” (1295).

[6] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (3599).

[7] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (3151).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 35-39
  • Imechapishwa: 13/09/2021