03. Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah

Jua – Allaah Akurehemu – ya kwamba at-Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah (Subhaanah) kwa ´Ibaadah na ndio dini ya Mitume ambao Allaah aliwatuma kwayo kwa waja Wake. Wa kwanza wao ni Nuuh (´alayhis-Salaam).

MAELEZO

Tambua masuala haya makubwa na uyaweke katika kumbukumbu yako na mambo unayoyatilia umuhimu daima na maishani. Nayo si mengine ni kwamba Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah na sio kumpwekesha Allaah katika uola (Rubuubiyyah). Hili lilifanywa na washirikina lakini hata hivyo halikuwafanya wakawa wapwekeshaji kwa kuwa hawakumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah. Kukubali kwao Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah sio ambayo inatakikana. Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah inafahamishwa na Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na ni yenye kulazimiana nayo. Kwa msemo mwingine ni kwamba yule mwenye kukubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah basi inamlazimu kuikubali Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Katika Aayah nyingi za Qur-aan Allaah anataja Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah hali ya kuwa ni yenye kufahamishwa na Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kumcha Allaah; ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa na akateremsha kutoka mbinguni maji akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi, msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua.” (02:21-22)

Hii ndio Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah inayofahamishwa na Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Akawa (Subhanaah) amesimamisha hoja dhidi yao katika yale wanayokanusha katika Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah kwa sababu ya yale wanayokubali katika Tawhiyd-ur-Ruubiyyah ili waweze kushikamana na hilo. Amewaambia ni vipi watakubali kuwa Yeye ndiye Muumbaji, Mruzukaji, Muhuishaji, Mfishaji na kwamba hana mshirika katika hayo halafu wanamshirikisha katika ´ibaadah.

Kuhusu wale wanaosema kuwa Tawhiyd ni kukubali ya kwamba Allaah ndiye Muumbaji, Mruzukaji, Muhuishaji, Mfishaji n.k. wanakosea kosa kubwa na hawakuleta Tawhiyd inayotakikana ambayo Mitume walilingania kwayo. ´Aqiydah za wanafalsafa wengi ambazo ndizo zenye kufunzwa hivi sasa katika masomo mengi ya Kiislamu wanafuata mfumo huu. Malengo ya Shaykh (Rahimahu Allaah) kuleta maana hii ni kutaka kuwaraddi watu hawa ambao wametilia bidii zao katika Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na wameiacha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Huu ndio utata wao wa kwanza ambapo wamefanya Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ndio Tawhiyd inayotakikana na kwamba yule mwenye kumpwekesha Allaah kwayo ndio mpwekeshaji. Wametunga vitabu juu yake, wakaujenga mfumo wao juu yake na wakatumia juhudi zao zote ili kuihakikisha.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 11
  • Imechapishwa: 08/10/2016