02. Kumzungumzisha vizuri yule unayemfunza na kumuombea du´aa

Jua – Allaah Akurehemu –

MAELEZO

Neno hili huanzwa kwa ajili ya kuzindua mambo muhimu. Pale unapotaka kumzindua mtu juu ya jambo muhimu katika mambo ya kielimu unamwambia “Tambua”. Lengo ni ili aweze kuzinduka. Imekuja katika fomu ya kuamrisha. Kwa msemo mwingine maana yake ni tambua yanayofuata, yatilie umuhimu na yatie akilini mwako yale unayotaka kuambiwa au kuandikiwa. Ni neno linaloletwa kuonyesha umuhimu wa yale yanayokuja baada yake. Amesema (Ta´ala):

لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

“Ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni Qadiyr (Muweza), na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi (Wake).” (65:12)

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

“Basi jua ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako na kwa ajili ya waumini wa kiume na waumini wa kike.” (47:19)

اعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ وَأَنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

”Jueni kuwa Allaah ni Mkali wa kuakibu na kwamba Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.” (05:98)

فَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَاعْلَمُوا أَنَّمَا عَلَىٰ رَسُولِنَا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ

”Mkikengeuka, basi jueni kwamba juu ya Rasuli Wetu ni (jukumu tu la) kufikisha ujumbe bayana.” (05:92)

Hili ni neno kubwa linaloletwa kwa ajili ya kutilia umuhimu. Halafu akasema:

“Allaah akurehemu.”

Hii ni du´aa Shaykh (Rahimahu Allaah) anamuombea kila mwenye kusoma kitabu hiki. Huku ni kwa ajili ya kumfanyia upole mwanafunzi na kuzungumza naye kwa uzuri ili mwanafunzi aweze kukubali.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 10
  • Imechapishwa: 08/10/2016