Kwa Jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

MAELEZO

Ameanza Kitabu kwa Basmalah, jambo ambalo ndio Sunnah. Vitabu vinatakiwa kuanzwa kwa Basmalah. Hivyo ndivyo Allaah amekianza Kitabu Chake. Ukifungua msahafu kitu cha kwanza utachoona ni:

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Kwa Jina la Allaah Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Himidi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.” (01:01-02)

Vilevile kabla ya kila Suurah kuna:

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

“Kwa Jina la Allaah Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akianza barua zake kwa Basmalah[1]. Tazama “as-Swahiyh” ya Imaam al-Bukhaariy (04/402) kitabu kuhusu Jihaad mlango “Du´aa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Uislamu, utume na kwamba baadhi yetu wasiwafanye wengine kuwa ni waungu badala ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

مَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُؤْتِيَهُ اللَّـهُ

“Haiwi kwa mtu ambaye Allaah amempa Kitabu… “(03:79)

Tazama pia katika “al-Fath” (06/109).

Tazama upambanuzi wa hilo katika “Zaad-ul-Ma´aad” ya Ibn-ul-Qayyim (03/688-696) alipokuwa akizungumzia uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi anapowaaandikia barua wafalme na wengineo.

Alipokuwa anataka kuwazungumzisha Maswahabah wake basi anaanza kikao chake kwa Basmalah.

Hekima ya kuanza kwa Basmahlah ni kwa ajili ya kutabaruku kwayo. Kwa kuwa ni neno lenye baraka. Mtu akianza na neno hili mwanzoni mwa kitabu au barua inakuwa na baraka. Vitabu au barua zisizoanza kwa Basmlah zinakuwa hazina kheri yoyote ndani yake.

Kwa mtamzo mwingine kuleta Basmalah ndani yake kuna kumtaka msaada Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hiyo ´Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu` maana yake ni kwamba naomba msaada na baraka kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Mwingi wa rehema (ar-Rahmaan) na Mwenye kuremu (ar-Rahiym) ni majina mawili mazuri kabisa ya Allaah. Yamebeba sifa ya huruma.

[1] al-Bukhaariy (2782), Muslim (1773), at-Tirmidhiy (2717) na Ahmad (01/263).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 9
  • Imechapishwa: 08/10/2016