3- ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nilikuwa naumwa ugonjwa wa bawasili nikamuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akanambia: “Swali kwa kusimama. Usipoweza, kwa kukaa. Usipoweza, kwa kulalia ubavu.”[1]

Amesema vilevile:

“Nilimuuliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) swalah ya mtu hali ya kukaa. Akasema: “Kuswali kwa kusimama ndio bora. Anayeswali kwa kukaa anapata nusu ya thawabu za ambaye ameswali kwa kusimama. Anayeswali kwa kulala [na katika upokezi mwingine “anayeswali chali”] anapata nusu ya thawabu za ambaye ameswali kwa kukaa.”[2]

Makusudio ya mgonjwa. Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka akawakuta watu wanaswali kwa kukaa kwa sababu ya maradhi. Akawaambia: “Swalah ya anayeswali kwa kukaa anapata nusu ya thawabu za ambaye anaswali kwa kusimama.”[3]

Alimtembelea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mgonjwa akamkuta anaswali juu ya mto. Akauchukua na akautupa. Akachukua fimbo ili aswali juu yake. Nayo akaichukua, akaitupa na kusema:

“Swali juu ya ardhi ukiweza. Usipoweza, fanya ishara na ufanye kusujudu kwako kuwe ni kwa kuinama chini zaidi kuliko kurukuu kwako.”[4]

[1] al-Bukhaariy, Abu Daawuud na Ahmad.

[2] al-Bukhaariy, Abu Daawuud na Ahmad. al-Khattwaabiy amesema:

“Makusudio ya Hadiyth ya ´Imraan ni yule mgonjwa anayeweza kustahamili na akasimama kwa tabu. Inajuzu kwake kukaa, lakini yule mwenye kukaa anapata nusu ya thawabu za yule mwenye kusimama, kwa ajili ya kumshaji´isha kusimama.”

Haafidhw Ibn Hajar amesema:

“Ni tafsiri yenye kuzingatiwa.” (Fath-ul-Baariy (02/468))

[3] Ahmad na Ibn Maajah kwa isnadi Swahiyh.

[4] at-Twabaraaniy, al-Bazzaar, Ibn-us-Simaak katika ”al-Hadiyth” (2/67) na al-Bayhaqiy kwa isnadi Swahiyh, kama nilivyobainisha katika ”as-Swahiyhah” (323).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 68-69
  • Marejeo: Firqatunnajia.com
  • Imechapishwa: 08/10/2016