03. Namna hii ndio tumaamini juu ya upwekekaji wa Allaah

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

Tunasema kuhusu upwekekaji wa Allaah hali ya kuwa ni wenye kuitakidi kwa tawfiyq ya Allaah ya kwamba:

1 – Allaah ni mmoja asiyekuwa na mshirika.

2 – Hakuna kitu mfano Wake.

3 – Hakuna chenye kumshinda.

4 – Hapana mungu wa haki asiyekuwa Yeye.

5 – Yeye ni wa kale[1] asiyekuwa na mwanzo, wa daima asiyekuwa na mwisho.

MAELEZO

Anasifiwa (Subhaanah) ukale kwa njia ya maelezo. Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Mlango kutoa maelezo zaidi ni mpana zaidi kuliko mlango wa sifa ambao unatakiwa kujengeka juu ya dalili.”[2]

Wanachuoni hawataji wa Kale (القديم) kwamba ni miongoni mwa majina mazuri ya Allaah. Hata hivyo wanalitumia jina hilo kwa njia ya kumtolea maelezo (Subhaanah). Amesema:

Yeye ni wa Kale, ambaye daima yuko na sifa Zake

Ni Mmoja bali Mwenye wema daima[3]

[1] Wa Kale haikuthibiti katika majina ya Allaah mazuri, kama alivyozindua hilo mshereheshaji (Rahimahu Allaah). Wanafalsafa wengi wamelitaja ili kuthibitisha uwepo Wake kabla ya kila kitu. Majina ya Allaah hayathibitishwi isipokuwa kwa dalili ya Qur-aan na Sunnah. Haijuzu kuthibitisha chochote katika hayo isipokuwa kwa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Maimamu wa Salaf wamethibitisha kwamba haijuzu kuthibitisha jina lolote kwa mapendekezo ya mtu. Wa Kale halifahamishi ile maana wanayoikusudia wanafalasafa. Kwa sababu kwa mujibu wa lugha ya kiarabu linaweza kuwa na maana ya ´wa kwanza` ingawa hakuwepo hapo kabla.  Allaah (Subhaanah) amesema:

وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ حَتَّىٰ عَادَ كَالْعُرْجُونِ الْقَدِيمِ

“Mwezi Tumeukadiria vituo mpaka ukarudi mwembamba kama karara kongwe.” (36:39)

Linafahamisha maana ya haki kwa ziada iliyotajwa na mtunzi pale aliposema:

“Yeye ni wa kale[1] asiyekuwa na mwanzo.”

Lakini halitakiwi kuzingatiwa kuwa ni miongoni mwa majina mazuri ya Allaah kwa sababu halikuthibiti kwa upande wa maandiko. Linatoshelezwa na jina la Allaah (Subhaanah) wa Kwanza. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ

“Yeye ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho.” (57:3)

[2] Badaa-i´-ul-Fawaa-id (1/162).

[3] an-Nuuniyyah (2/37).

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad bin ´Abdil-´Aziyz bin Maaniy´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haashiyah ´alaa al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 18-21
  • Imechapishwa: 10/11/2021