03. Mtaulizwa juu ya tende na maji

12 – Ishaaq ametuhadithia: [tupu] ametuhadithia: Hishaam ametuhadithia, kutoka kwa al-Hasan, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Naapa kwa Ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake! Familia ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haijapatapo kushiba siku tatu… ”

al-Hasan amesema:

”Hakuyasema hayo kwa ajili ya kuwalalamikia watu, isipokuwa ni kwa ajili ya kujipa udhuru.”

13 – ´Aliy bin al-Ja´d ametuhadithia: Abu Ghassaan ametuhadithia, kutoka kwa Ibn Abiy Haazim, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Yaziyd bin Haaruun, kutoka kwa ´Urwah, kutoka kwa ´Aaishah, ambaye amesema:

”Miezi miandano miwili ilikuwa inaweza kutupitia bila ya kuwashwa moto katika nyumba miongoni mwa nyumba za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Nikasema kumwambia shangazi yangu: ”Sasa mlikuwa mnaishi kwa kitu gani?” Akasema: ”Vieusi viwili; maji na tende.”[1]

14 – ´Abdur-Rahmaan bin Swaalih al-´Atakiy ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Muhammad al-Muhaaribiy ametuhadithia, kutoka kwa Yahyaa bin ´Ubaydillaah al-Madaniy, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anhumaa), ambaye amesema:

”Siku moja nilipitwa na chakula cha jioni ambapo nikarudi nyumbani na kusema: ”Je, hamna chakula cha jioni?” Wakasema: ”Hapana.” Nikalala kwenye kitanda changu na nikaanza kujigeuza huku na kule na usingizi hauji kutokana na njaa. Nikafikiria kwenda msikitini kuswali na kujishughulisha mpaka kupambazuke. Nikafanya hivo na nikaswali kile kiasi alichotaka Allaah. Baadaye nilijiegemeza kwenye kona moja ya msikiti. Tahamaki akajitokeza ´Umar na kusema: ”Hakuna kilichonitokea isipokuwa kile kilichokutoa wewe.” Tulipokuwa katika hali hiyo tahamaki akajitokeza kwetu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: ”Hakuna kilichonitokea isipokuwa kile kilichokutoeni. Nifuateni twende al-Waaqimiy.” Tukatoka katika mwanga wa mwezi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia mke wake: ”Yuko wapi mume wako?” Akasema: ”Ameende kutuletea maji tamu kutoka kwenye chemchem ya Banuu Haarithah.” Akaja amebeba chombo chake cha maji na akakitundika kwenye mtende. Kisha akatugeukia na kusema: ”Karibuni! Sijawahi kutembelewa na watu kama walionitembelea usiku huu.” Akaenda kukata rundo la tende, akachukua kisu na akaingia walipo kondoo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Usimchukue kondoo mwenye maziwa” au ”Usimchukue mwenye chuchu”. Akamchinja, akamchuna na akamwamrisha mke wake kukanda unga na kutengeneza mkate. Akaikata ile nyama na kuitupa kwenye sufuria, akawasha moto chini yake na akafanya uji uliowekwa kwenye mchuzi na nyama. Kisha akatuhudumia mbele yetu. Tukala mpaka tukashiba. Kisha akasimama kwenda kwenye chombo cha maji, kilichokuwa kimepozwa kutokana na upepo. Akatumiminia ndani ya chombo, ambapo akampokeza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akanywa. Kisha Abu Bakr kisha ´Umar. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Himdi zote njema ni za Allaah ambaye ametutoa – na hakuna kilichotutoa isipokuwa njaa – kisha hatukurudi mpaka tumeyapata haya. Hakika mtaulizwa juu ya haya siku ya Qiyaamah. Kwani hizi ni katika neema.”[2]

[1] al-Bukhaariy (5383) na Muslim (2972-2976).

[2] Muslim (2038), at-Tirmidhiy (2369) na at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” (567).

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 32-35
  • Imechapishwa: 05/06/2023