5 – Khalid bin Khidaash ametuhadithia: Hammaad bin Zayd ametuhadithia, kutoka kwa Mujaalid, kutoka kwa ash-Sha´biy, kutoka kwa Masruuq, ambaye ameeleza:

”Niliingia kwa ´Aaishah, akaniita kwenye chakula na kusema: ”Kula. Ni mara chache hula nikashiba. Endapo ningelipenda kulia, basi ningelia.” Nikasema: ”Kwa nini?” Akasema: ”Naikumbuka ile hali ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliacha dunia akiwa nayo. Hakupatapo kushiba mkate wa ngano mara mbili mpaka pale alipokutana na Allaah.”[1]

6 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Muhammad bin Khaazim ametuhadithia: al-A´mash ametuhadithia, kutoka kwa Ibraahiym, kutoka kwa al-Aswad, kutoka kwa ´Aaishah, ambaye amesema:

”Hakupatapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kushiba mkate siku tatu mfululizo mpaka alipoaga dunia.”[2]

7 – Ishaaq bin Ibraahiym ametuhadithia: ´Abdus-Swamad bin ´Abdil-Waarith ametuhadithia: Shu´bah ametuhadithia, kutoka kwa Abu Ishaaq, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Zayd, kutoka kwa al-Aswad, kutoka kwa ´Aaishah, ambaye amesema:

”Hakupatapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kushiba mkate wa shayiri siku mbili mpaka alipokufa.”

8 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa Ibraahiym, kutoka kwa al-Aswad, kutoka kwa ´Aaishah, ambaye ameeleza:

”Tangu alipofika Madiynah, familia ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haijapatapo kushiba mkate wa ngano siku tatu mfululizo mpaka alipokufa.”[3]

9 – Ishaaq bin Ibraahiym ametuhadithia: Rawh ametuhadithia: Shu´bah ametuhadithia, kutoka kwa Simaak bin Harb: Nimemsikia an-Nu´maan bin Bashiyr akisema:

”´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alizungumza yale yaliyowapata watu katika mambo ya kidunia na akasema: ”Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameinama siku nzima kwa kutopata kitu cha kulijaza tumbo lake katika tende.”[4]

10 – Ishaaq bin Ibraahiym ametuhadithia: [tupu] ametuhadithia: Ismaa´iyl bin ´Abdil-Malik ametuhadithia, kutoka kwa Abuz-Zubayr, kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah, ambaye amesema:

”Ilipokuwa siku ya vita vya Khandaq nilimtazama Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nikamuona jinsi alivyofunga kijiwe ndani ya kikoi chake ili kuunyosha sawa mgongo wake kutokana na njaa.”[5]

11 – [Tupu] Zaynab [tupu], kutoka kwa Hayyaan bin Juz’, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akinyoosha sawa mgongo wake kwa kufunga tumbo lake kijiwe kutokana na njaa.”

[1] at-Tirmidhiy (2357) ambaye amesema:

”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

[2] Muslim (2970).

[3] al-Bukhaariy (5374) na Muslim (2970).

[4] Muslim (2978).

[5] al-Haythamiy amesema:

”Ameipokea Abu Ya´laa. Wapokezi wake ni waaminifu licha ya udhaifu wa Ismaa´iyl bin ´Abdil-Malik.” (Majma´-uz-Zawaa-id (10/317))

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 28-31
  • Imechapishwa: 05/06/2023