Kuhusu matendo ya ulimi, amesema (Ta´ala):

يَسْتَخْفُونَ مِنَ النَّاسِ وَلَا يَسْتَخْفُونَ مِنَ اللَّـهِ وَهُوَ مَعَهُمْ إِذْ يُبَيِّتُونَ مَا لَا يَرْضَىٰ مِنَ الْقَوْلِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطًا

”Wanajificha watu wasiwaone na wala hawajifichi kwa Allaah ilihali yupamoja nao pale wanapokesha kupanga njama kwa maneno asiyoyaridhia. Na Allaah daima kwa yale wayafanyayo ni Mwenye kuyazunguka.”[1]

Akataja maneno yao kwanza, kisha akayataja kuwa ni matendo.

Amesema tena (Ta´ala):

وَإِن كَذَّبُوكَ فَقُل لِّي عَمَلِي وَلَكُمْ عَمَلُكُمْ ۖ أَنتُم بَرِيئُونَ مِمَّا أَعْمَلُ وَأَنَا بَرِيءٌ مِّمَّا تَعْمَلُونَ

”Na wakikukadhibisha, basi sema: “Mimi nina matendo yangu, nanyi mna matendo yenu. Nyinyi hamna dhimma na yale niyatendayo, na wala mimi sina dhimma na yale myatendayo.”[2]

Matendo ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yalikuwa yepi kama sio kuwaombea du´aa kwa Allaah? Kule kumkadhibisha kwao hapa amekuita kuwa ni matendo.

Amesema (Tabaarak wa Ta´ala) mahala kwengine:

قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ إِنِّي كَانَ لِي قَرِينٌ يَقُولُ أَإِنَّكَ لَمِنَ الْمُصَدِّقِينَ أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَدِينُونَ قَالَ هَلْ أَنتُم مُّطَّلِعُونَ فَاطَّلَعَ فَرَآهُ فِي سَوَاءِ الْجَحِيمِ قَالَ تَاللَّـهِ إِن كِدتَّ لَتُرْدِينِ وَلَوْلَا نِعْمَةُ رَبِّي لَكُنتُ مِنَ الْمُحْضَرِينَ أَفَمَا نَحْنُ بِمَيِّتِينَ إِلَّا مَوْتَتَنَا الْأُولَىٰ وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ لِمِثْلِ هَـٰذَا فَلْيَعْمَلِ الْعَامِلُونَ

“Aseme msemaji mmoja katika wao: “Hakika mimi nilikuwa na rafiki mwandani aliyekuwa akiniambia: Je, hivi wewe ni miongoni mwa wanaosadikisha, je, tutakapokufa, tukawa udongo na mifupa, eti kweli sisi tutahukumiwa?” Atasema: “Je, mngependa kuchungulia?” – Basi akapitisha macho, akamuona [rafiki yake] yuko katikati moto uwakao vikali mno akasema: “Naapa kwa Allaah! Ulikaribia kuniangamiza; na lau kama si neema ya Mola wangu, bila shaka ningelikuwa miongoni mwa wahudhurishwao! Je, sisi hatutakufa tena? Isipokuwa kifo chetu cha kwanza, nasi hatutaadhibiwa. Hakika huku ndiko kufuzu kukubwa! Kwa mfano wa haya basi watende wenye kutenda!”[3]

Kuko wapi kusadikisha kama si yale maneno? Pamoja na hivyo mzungumzaji ameyaita kuwa ni matendo.

Vilevile amesema (Ta´ala):

اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ

“Tendeni, enyi familia ya Daawuud, kwa shukurani!” Na ni wachache miongoni mwa waja Wangu wenye kushukuru.”[4]

Kile kinachojulikana kwa watu wengi ni kwamba shukurani imefungamana na kuhimidi na kusifu kwa ulimi, ingawa kulipiza wema pia kunaweza kuitwa kuwa ni kushukuru.

Yote haya ambayo tumefasiri ni yenye kuafikiana na udhahiri wa Qur-aan na tafsiri za wanazuoni. Haya ndio yaliyoenea na yaliyohifadhiwa katika maneno ya waarabu. Kwa mfano wanaweza kusema kuwa fulani hii leo amefanya mambo mengi na huku wakikusudia kuwa amezungumza ya kweli na kutoa ushahidi siku hiyo. Mtu akimweleza mwingine mambo yanayochukiza, wanaweza kusema kuwa amefanya mambo ya kutisha. Wakaita kuwa ni matendo ijapo hakufanya isipokuwa kuzungumza peke yake. Vilevile Hadiyth isemayo:

“Yule mwenye kujumuisha maneno yake katika kitendo chake, huwa machache maneno yake isipokuwa katika yale yenye kumnufaisha.”[5]

Tunaona namna ambavyo Qur-aan, Sunnah, maneno ya wanazuoni na mtazamo sahihi vyote vinathibitisha ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah kuhusu imani. Maoni mengine yanabaki kivyake. Kipi cha kufuatwa baada ya hoja hizi nne?

[1] 4:108

[2] 10:41

[3] 37:51-61

[4] 34:13

[5] Sijayapata. Dhana yangu kubwa ni kwamba ni maneno ya Swahabah.

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 54-57
  • Imechapishwa: 26/06/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy