Watu wa maoni yanayosema kuwa imani inakamilika kwa kule tu kuitamka wanaweza kulazimika kuingia katika jambo baya zaidi kuliko tuliyoyataja. Kwa mfano tunajua kuwa Allaah alisema kuhusu Ibliys wakati alipomwamrisha amsujudie Aadam:

إِلَّا إِبْلِيسَ اسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ

“… isipokuwa Ibliys, alitakabari na akawa katika makafiri.”[1]

Allaah akasema kuwa amekuwa kafiri kwa kule kufanya kwake kiburi, licha ya kwamba anamtambua Yeye na si mwenye kumkanusha. Hukumsikia akisema:

خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ

“Umeniumba kwa moto na yeye umemuumba kwa udongo.”[2]

رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ

”Ee Mola! Kwa vile umenihukumia kupotoka, basi hakika nitawapambia katika ardhi na nitawapotoa wote”?[3]

Amekubali kuwa Allaah ndiye Mola Wake na akathibitisha makadirio pale aliposema:

بِمَا أَغْوَيْتَنِي

”Kwa vile umenihukumia kupotoka… ”

Pengine baadhi wakafasiri kwamba alikuwa kafiri kabla ya hapo, sioni msingi wowote wa mtazamo huo. Kwa sababu kama angelikuwa kafiri kabla ya kuamrishwa kumsujudia Aadam, basi asingelikuwa pamoja na Malaika[4]. Wala asingelikuwa mwenye kuasi kama hakuwa miongoni mwa walioamrishwa kusujudu. Kwa mujibu wa maoni haya yanapelekea kwamba Ibliys amerudi katika imani baada ya kufuru kwa sababu alisema:

رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي

“Mola wangu! Kwa vile Umenihukumia kupotoka… ”[5]

خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ

”Umeniumba kutokana na moto naye umemuumba kutokana na udongo.”

Je, inawezekana kwa ambaye anamtambua Allaah, Kitabu Chake na yaliyokuja kutoka kwa Allaah kudai hii leo kuwa Ibliys aliamini?

[1] 02:34

[2] 7:12

[3] 15:39

[4] Bi maana pamoja na wale walioamrishwa kumsujudia Aadam. Mtunzi (Rahimahu Allaah) hakusudii kwamba alikuwa pamoja na Malaika katika maumbile na sifa. Anawezaje kufanya hivo ilihali Qur-aan inasema:

كَانَ مِنَ الْجِنِّ فَفَسَقَ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِ

“Alikuwa miongoni mwa majini akaasi amri ya Mola wake.” (18:50)?

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Malaika wameumbwa kutokana na nuru. Majini wameumbwa kutokana na moto. Aadam ameumbwa kutokana na kile mlichoelezwa.” (Muslim)

[5] 15:39

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 57-59
  • Imechapishwa: 26/06/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy