Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

ya kwamba ni wajibu juu yetu kujifunza masuala manne:

1 – Ujuzi, nao ni ujuzi wa kumjua Allaah, ujuzi wa kumjua Mtume Wake na ujuzi wa kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili.

MAELEZO

Bi maana kuwa na uhakika na yakini – usiwe na mashaka na dhana – ya kwamba ni lazima kwako – na si jambo la kupendeza tu – kujifunza mambo haya manne. Usipojifunza basi unapata dhambi. Kwa kuwa jambo la lazima ni lile ambalo analipwa thawabu yule mwenye kulifanya na anaadhibiwa yule mwenye kuliacha[1]. Kwa hiyo ukijifunza mambo haya manne basi wewe ni mwenye kulipwa thawabu. Ukiacha kujifunza utaadhibiwa. Yule mwenye kuacha kujifunza nayo ni mwenye kupata dhambi na mtenda maasi kwa sababu ameenda kinyume na jambo la lazima. Kisha imamu ikaanza kutaja mambo haya manne kwa njia ya ujumla akasema:

1 – Ujuzi. Akafasiri (Rahimahu Allaah) kuwa ni kumtambua Allaah, kumtambua Mtume Wake na kuijua dini ya Uislamu kwa dalili. Mambo haya yanakulazimu. Utambuzi wa kumjua Allaah ni kujua majina, sifa Zake na kwamba Yeye (´Azza wa Jall) yupo, kwamba yuko juu ya ´Arshi, kwamba anayo majina mazuri na sifa kuu ambazo amejiita kwazo Mwenyewe na amemwita kwazo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Vilevile mtu anatakiwa kuwa na utambuzi ya kwamba Allaah ndiye Mola na wengine wote ni waja, kwamba Yeye ni Muumba na wengine wote ni viumbe, ya kwamba Yeye ni Mfalme na wengine wote ni wenye kumilikiwa, ya kwamba Yeye ni Mwenye kuyaendesha mambo na wengine wote ni wenye kuendeshwa.

Aidha mtu anatakiwa kuwa na ujuzi ya kwamba Yeye ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa na hakuna mwingine anayestahiki. ´Ibaadah ni yale maamrisho na makatazo. Kwa msemo mwingine unafanya maamrisho na unaacha makatazo. Maana nyingine ya ´ibaadah ni jina lililokusanya yale yote anayoyapenda Allaah na kuyaridhia katika maneno, matendo yaliyojificha na yaliyo wazi[2]. Ukiyajua haya basi utazingatiwa kuwa umemtambua Allaah (´Azza wa Jall). Allaah ndiye anastahiki ´ibaadah zote kama vile swalah, zakaah, swawm, hajj, du´aa, kichinjwa, nadhiri, kuomba uokozi, kuomba msaada, utegemezi, khofu na matarajio. Aina hizi atazibainisha mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah).

Maana ya utambuzi wako kuwa Allaah ndiye mwenye kustahiki ni kwamba unatakiwa kujua kuwa Yeye ndiye anastahiki kuabudiwa na haijuzu kumwelekezea mwengine. Allaah hayuko radhi aabudiwe mwengine. Ni mamoja huyo anayeabudiwa ni Malaika aliye karibu wala Mtume aliyetumwa, ambao ndio viumbe wabora zaidi. Usimfanyie ´ibaadah Jibriyl, Malaika mwingine, Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Mitume wengine (SwallaAllaahu ´alayhim wa sallam). Haki ya Mtume ni kumtii, kumpenda na kumtukuza. Hata hivyo hana haki ya kuabudiwa na kukusudiwa kwayo. Hapo utazingatiwa umemtambua Allaah.

[1] Tazama ”al-Bahr-ul-Muhiytw fiy Usuwl-il-Fiqh” (01/140), ”at-Tahbiyr Sharh-it-Tahriyr” (02/715), ”at-Taqriyr wat-Tahbiyr” (02/152) na ”al-Mahsuwl” (01/118) ya ar-Raaziy.

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/149).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 30/01/2023