Masimulizi ya Ibn ´Abbaas yaliyopokelewa na al-Bukhaariy katika kubainisha sababu ya kuzuka kwa shirki katika watu wa Nuuh tunapata faida zifuatazo:

1 – Ukhatari wa kutundika picha ukutani na kusimamisha masanamu katika mabaraza na viwanja na kwamba hilo mwishoni huwapelekea watu katika shirki. Hali hiyo itawavuta kidogo kidogo kuzitukuza picha hizo na masanamu kwa kuziabudu na kuamini kuwa zinaleta kheri na kuzuia shari, kama ilivyotokea kwa watu wa Nuuh.

2 – Bidii kubwa ya shaytwaan katika kumpotosha mwanaadamu na kumpangia njama. Wakati mwingine anatumia hisia za watu na madai ya kuwapendezea kheri. Alipoona watu wa Nuuh wakipenda sana watu wema, ndipo aliwahamasisha kupitiliza katika mapenzi haya kwa namna ya kuwaamrisha kuweka picha zao mahali wanapokaa. Malengo yake juu ya hili ni kuwatoa katika njia ya sawa.

3 – Shaytwaan hapangi njama zake kwa kizazi kilichopo tu, bali pia anawalenga vizazi vijavyo. Aliposhindwa kueneza ushirikina kwa kizazi cha sasa cha watu wa Nuuh, akawa na matumaini na kutengeneza mitego juu ya vizazi vijavyo.

4 – Haijuzu kuchukulia wepesi njia za shari, bali ni wajibu kuzikata na kufunga milango yake.

5 – Ubora wa wanazuoni wanaoifanyia kazi elimu yao. Kule kuwa kwao kati ya watu ni kheri na kukosekana kwao kati yao ni shari. Hakika shaytwaan hakuweza kuwapotosha watu wa Nuuh isipokuwa mpaka walipokosekana.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 08-09
  • Imechapishwa: 01/01/2025