Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti za swalah ni tisa:

1 –  Mtu kuwa Muislamu.

2 – Mtu kuwa na akili.

3 – Mtu kuwa na uwezo wa kupambanua.

4 – Mtu kutokuwa na hadathi.

5 – Mtu kuondosha najisi.

6 – Kufunika viungo ambavyo havitakiwi kuonekana (´Awrah).

7 – Kuingia kwa wakati.

8 – Kuelekea Qiblah.

9 – Nia.

Sharti ya kwanza ni Uislamu na kinyume chake ni ukafiri (Kufr). Matendo ya kafiri ni yenye kurudishwa, bila ya kuzingatia sawa akifanya ´amali yoyote ile. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

مَا كَانَ لِلْمُشْرِكِينَ أَن يَعْمُرُواْ مَسَاجِدَ الله شَاهِدِينَ عَلَى أَنفُسِهِمْ بِالْكُفْرِ أُوْلَئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ وَفِي النَّارِ هُمْ خَالِدُونَ

“Si haki kwa washirikina kuamirisha misikiti ya Allaah hali ya kuwa wanajishuhudia nafsi zao kwa ukafiri. Hao yamebatilika matendo yao na katika Moto wao ni wenye kudumu.”[1]

وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاء مَّنثُورًا

”Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya matendo yoyote yale na Tutayafanya kuwa ni mavumbi yaliyotawanyika.”[2]

MAELEZO

Sharti ya kwanza – Miongoni mwa sharti za swalah ni pamoja na Uislamu. Uislamu maana yake ni kule kujisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujiepusha na shirki na washirikina. Mtu ameitwa kuwa ni ´muislamu` kwa sababu ni mwenye kujisalimisha na mwenye kunyenyekea Shari´ah na dini ya Allaah. Ni mwenye kunyenyekea amri za Allaah. Muislamu ni yule mwenye kujisalimisha kwa Allaah na si kwa mwengine. Mshirikina ni yule ambaye anajisalimisha kwa Allaah na kwa mwengine. Kafiri ni yule ambaye anafanya inda ya kumwabudu Allaah. Mshirikina na mwenye kufanya kiburi wote wawili ni makafiri.

Msingi wa dini ya Uislamu ni kumshuhudilia Allaah juu ya upwekekaji na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya ujumbe. Nako ni kule mtu kutamka kwamba anashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Mtu anaingia ndani ya Uislamu na kutoka duniani kwa maneno hayo mawili. Mtu akitamka shahaadah mbili, akajisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha na akanyenyekea Shari´ah Yake ndipo swalah yake inasihi.

[1] 09:17

[2] 25:23

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 09-10
  • Imechapishwa: 01/12/2021