Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti za swalah ni tisa:

1 – Mtu kuwa Muislamu.

2 – Mtu kuwa na akili.

3 – Mtu kuwa na uwezo wa kupambanua.

4 – Mtu kutokuwa na hadathi.

5 – Mtu kuondosha najisi.

6 – Kufunika viungo ambavyo havitakiwi kuonekana (´Awrah).

7 – Kuingia kwa wakati.

8 – Kuelekea Qiblah.

9 – Nia.

MAELEZO

Hizi ndio sharti za swalah kwa ujumla. Sharti ni kitu ambacho ni lazima kiwepo. Kusipokuwepo sharti, basi hakuna pia kile kinachoshurutishwa. Lakini kwa vile sharti imepatikana haina maana kwamba ni lazima vilevile kupatikane kitendo[1]. Kukikosekana sharti basi kunakosekana vilevile kile kilichoshurutishwa. Ikiwa moja katika masharti haya tisa itakosekana basi swalah haisihi. Lakini ikiweko basi pengine swalah ikaweko au isiweko. Kwa mfano kutawadha ni moja ya kusihi kwa swalah. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hakubali swalah ya mmoja wenu pindi anapopata hadathi mpaka atawadhe.”[2]

Kukikosekana wudhuu´ basi hakuna swalah pia. Lakini wudhuu´ unaweza kuweko na swalah ikaweko au isiweko. Mtu anaweza kutawadha ambapo akaswali au pengine vilevile asiswali. Lakini swalah haisihi isipokuwa mpaka kwa kuweko wudhuu´. Sharti ni ile ambayo inatangulia kile kilichowekewa sharti. Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sharti za swalah ni tisa.”

Sharti za kusihi kwa swalah. Dalili zake zimepatikana kwa kufuatilia na kusoma. Kwa msemo mwingine ni kwamba wanachuoni wameyafuatilia maandiko na kuzikusanya sharti hizi na kuona ni tisa. Ni kama mfano wa mambo yaliyokatazwa wakati wa Ihraam kwa yule mwenye kuhirimia ambayo pia ni tisa. Dalili zake ni kule kufuatilia na kusoma. Hiyo ina maana kwamba wanachuoni wameyafuatilia maandiko na wakayadurusu na kuona kuwa makatazo aliyokatazwa anayefanya Ihraam anapohirimia hajj au ´umrah ni tisa:

1 – Kuvaa nguo ilioshonwa kwa mwanamme.

2 – Kufunika kichwa kwa mwanamme.

3 – Kunyoa nywele.

4 – Kukata kucha.

5 – Manukato.

6 – Kuua kiwindwa.

7 – Kufunga ndoa.

8 – Jimaa.

9 – Kustarehe kwa njia nyenginezo zisizokuwa tupu.

[1] Tazama ”at-Tahbiyr Sharh-it-Tahriyr” (03/1067) ya al-Mardaawiy.

[2] al-Bukhaariy (6954) na Muslim (225).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 7-8
  • Imechapishwa: 01/12/2021