02. Fadhila za kujifunza elimu ya dini

Kumekuja dalili nyingi zenye kubainisha fadhila za elimu ili kutia hamu na kuzivutia nafsi kupata jambo hilo kubwa. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ

“Hakika wanaomkhofu Allaah kihakika miongoni mwa waja Wake ni wasomi.”[1]

Hakika wale ambao wanamcha Allaah ukweli wa kumcha ni wanachuoni. Wanachuoni woga wao wa kumuogopa Allaah ni mkamilifu. Kwa kuwa maarifa yao ya kumjua Allaah ni kamilifu. Allaah (´Azza wa Jalla) amesema:

يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ

“Allaah atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu zaidi.”[2]

Wale ambao Allaah (´Azza wa Jall) kwanza amewaruzuku imani, kisha akawaruzuku pamoja na imani elimu, basi Allaah (´Azza wa Jall) atawanyanyua daraja za juu duniani na Aakhirah. Wao ndio wako juu na wenye kustahiku kusifiwa na walio na ujira mkubwa. Hapa kuna dalili kubwa ya kwamba elimu katika Uislamu inamfaa mtu pamoja na imani. Ambaye atakusanya pamoja na imani elimu, basi elimu hiyo itamnufaisha na Allaah atamnyanyua kwa elimu hiyo daraja za juu zaidi. Kuhusiana na mtu ambaye atakuwa na elimu peke yake pasi na imani, hakika hilo halitomnufaisha kitu na wala halitomfaa kitu. Bali itapotea bure. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ

“Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua?”[3]

Kunaulizwa kwa njia ya makemeo. Ni kama kwamba amesema: “Ee Muhammad! Waambie hawa wakaidi! Hivi kweli wanalingana wale wenye kujua na wale wasiojua? Waulize hali ya kuwakemea: Je, wanalingana wale wenye kujua na wale wasiojua sawa katika mizani ya akili, katika mizani ya werevu, katika mizani ya Shari´ah na katika mizani ya elimu? Hapana, ninaapa kwa Allaah ya kwamba hawalingani hata siku moja.”

Amekula khasara yule aliyedhania kwamba wasomi wako sawa na wengine. Amekula khasara na amekhalifu akili na dalili yule mwenye kudhania kwamba wale wasiojua – japokuwa watadai kuwa ni walinganizi na wakadai yakudai – ya kwamba wako sawa na wanachuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye atachukua njia akitafuta kwayo elimu, basi Allaah atamsahilishia kwayo njia ya kuelekea Peponi. Hawatokusanyika watu katika nyumba miongoni mwa nyumba za Allaah wakisoma Kitabu cha Allaah na wakikiduru baina yao isipokuwa Malaika huwafunika, huteremkiwa na utulivu, hufunikwa na rahmah na Allaah huwataja kwa wale walio Kwake.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth kubwa ambayo ndani yake amebainisha fadhila za elimu, kuanzia mwanzo hadi mwisho wake, yafuatayo:

“Yule ambaye atachukua njia akitafuta kwayo elimu, basi Allaah atamsahilishia kwayo njia ya kuelekea Peponi. Hakika Malaika huziweka mbawa zao juu ya mwanafunzi wakiridhia kile anachokifanya. Hakika mwanachuoni anaombewa msamaha na waliyoko mbinguni na ardhini mpaka samaki ndani ya maji. Ubora wa mwanachuoni juu ya mfanya ´ibaadah ni kama ubora wa mwezi juu ya nyota zingine. Hakika wanachuoni ndio warithi wa Mitume. Mitume hawakurithi dinari wala dirhamu, bali wamerithi elimu. Basi yule atakayeichukua, basi atakuwa amejipatia fungu kubwa kabisa.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anabainisha fadhila za elimu wakati wa kujifunza na kuitafuta.

Yule ambaye atachukua njia… – Mwenye kusafiri akaacha nyumbani kwao, familia yake na kula raha. Akaamua kusafiri. Kwa nini anasafiri?

… akitafuta kwayo elimu – Ndugu! Hapa kuna dalili juu ya kwamba elimu inatafutwa na kwamba elimu inafikiwa kwa mtu kufanya sababu.

basi Allaah atamsahilishia… – Wanachuoni wamesema: “Allaah atamfanyia wepesi wa njia ya kuelekea Peponi kwa mambo mawili:

La kwanza: Elimu kwa dhati yake yenyewe ni moja katika njia yenye kuelekeza Peponi. Hivyo basi, yule mwenye kuchukua njia akitafuta kwayo elimu, basi yuko katika moja ya njia zenye kuelekeza Peponi na ambayo inamfikisha mtu Peponi.

La pili: Mwenye kuchukua njia akitafuta kwayo elimu, basi Allaah atamsahilishia na kumuwepesishia ´ibaadah. Hivyo katika njia ya ´ibaadah anakuwa miongoni mwa waliotangulia.”

Kwa ajili hiyo wanasema baadhi ya waalimu zetu:

“Ukitaka kuona kama uko na Ikhlaasw katika kujifunza elimu, basi jitazame ´ibaadah zako. Ambaye ana Ikhlaasw katika kujifunza elimu, basi Allaah atamsahilishia njia ya kwenda Peponi. Miongoni mwa njia za kwenda Peponi ni ´ibaadah.”

Hakika Malaika huziweka mbawa zao… – Malaika ambao Allaah (´Azza wa Jall) amewaumba kwa ajili ya utiifu:

لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

“Hawamuasi Allaah kwa yale anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa.”[6]

Hakuna wanachopenda isipokuwa utiifu peke yake. Malaika huziweka mbawa zao juu ya mwanafunzi wakinyenyekea kwake. Sio kwa sababu mwanafunzi huyu ana hekima, mwerevu, mtukufu au kwa sababu ana mali nyingi. Bali ni kwa sababu ya kuridhia kile kinachofanywa na mwanafunzi huyu. Kwa sababu wanajua fadhila za elimu mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Hivyo wananyenyekea kwa mwanafunzi huyu wakiridhia kile anachokifanya. Yote hayo ni fadhila za mwanafunzi wakati anapoitafuta na akawa bado ni mwenye kuendelea kupita katika njia yake wakati wa kuitafuta. Ama akiwa ameshaipata elimu, huyo ana fadhila zake zingine na ni suala lingine. Inahusiana na daraja ya juu zaidi na zaidi.

Hakika mwanachuoni anaombewa msamaha… – Kila kilichoko mbinguni na ardhini basi kinamuombea msamaha mwanachuoni. Sivyo tu bali Allaah (´Azza wa Jall) anamswalia mwanachuoni na anamtaja kwa wema katika ulimwengu wa juu.

… mpaka samaki ndani ya maji – Hata wanyama wa ardhini wakiwemo samaki waliyomo ndani ya bahari wanamuombea msamaha mwanachuoni.

Ubora wa mwanachuoni juu ya mfanya ´ibaadah… – Haya ni kutokana na ada waliozowea watu ambapo wanaufadhilisha mwezi juu ya nyote zingine zote. Watu huona kuwa mwezi ndio nyota bora zaidi. Kadhalika mwanachuoni. Ubora wake juu ya mfanya ´ibaadah, asokuwa na elimu, ni kama mfano wa ubora wa mwezi juu ya nyota zingine zote.

Hakika wanachuoni ndio warithi wa Mitume – Wanachuoni ndio viumbe walio karibu zaidi na Mitume. Mwanaadamu anapofariki anarithiwa na warithi. Mitume wanapofariki wanachuoni ndio huwarithi. Wanachuoni ndio watu walio karibu zaidi na Mitume. Wanachukua elimu yao kutoka kwa Mitume. Hivyo wao ndio wako karibu na wao kihaki na kikweli.

Hakika wanachuoni hawakurithi… – Mambo hayo hukwisha na kuondoka. Wamerithi elimu inayobaki. Ambaye atachukua sehemu katika elimu, basi amechukua sehemu kubwa katika mirathi ya Mitume. Hii ni fadhila kubwa.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye Allaah anamtakia kheri, basi humpa ufahamu akaielewa dini.”[7]

Miongoni mwa alama zenye kuonesha kuwa Allaah (´Azza wa Jall) anamtakia mja Wake kheri, ni kuwa utamuona anajibidisha kutaka kuielewa dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Anajibidisha nafsi yake katika kujifunza elimu ili awe katika wasomi wa dini ya Allaah (´Azza wa Jall) wa kikweli.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fadhila za elimu ni bora zaidi kuliko fadhila za ´ibaadah.”[8]

Elimu ambayo si wajibu yenye kuzidi kile kiwango cha kujifunza elimu ya wajibu ni bora kuliko ´ibaadah za naafilah. Kwa ajili hiyo wanachuoni wamesema ya kwamba lau mwanafunzi atatatizika kusoma elimu na kufanya ´ibaadah ambazo ni za Sunnah, basi atatakiwa kutanguliza kusoma elimu mbele. Hakika kujifunza elimu ni bora kuliko ´ibaadah za Sunnah. Hilo ni kutokana na dalili ya Hadiyth hii tuliyosikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 40:28

[2] 58:11

[3] 39:09

[4] Muslim (2699)

[5] Abu Daawuud (3641), at-Tirmidhiy (2682), Ibn Maajah (223) na Ibn Hibbaan (88).

[6] 66:06

[7] al-Bukhaariy (71) na Muslim (1037)

[8] al-Haakim (01/171) na at-Twabariy katika “al-Awsatw” (3960). al-Albaaniy amesema katika “Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (01/16):

“Ni Swahiyh kutokana na zengine.”

 

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016