01. Ni yepi makusudio ya soksi za ngozi na soksi za kawaida? Ni ipi hukumu ya kupangusa juu yake?

Swali 1: Ni yepi makusudio ya soksi za ngozi na soksi za kawaida? Ni ipi hukumu ya kupangusa juu yake?

Jibu: Soksi za ngozi ni kile anachofaa mtu katika ngozi na mfano wake. Soksi za kawaida ni kile anachovaa mtu katika pamba na mfano wake.

Kupangusa juu yake ni miongoni mwa Sunnah iliopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa yule ambaye amevaa soksi basi bora ni kufuta juu yuke kuliko kuzivua kwa ajili ya kuosha miguu. Dalili ya hilo ni Hadiyth ya al-Mughiyrah bin Shu´bah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameelezea kuhusu wudhuu´ wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). al-Mughiyrah amesema:

“Niliinama ili kumvua soksi zake za ngozi akasem: “Ziache. Nilizivaa nikiwa katika hali ya twahara” na hivyo akapangusa juu yake.”

Upangusaji ni kitu kimethibiti ndani ya Qur-aan na Sunnah. Kuhusu Qur-aan, Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُؤُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ

“Enyi mlioamini!  Mnaposimama kwa ajili ya swalah, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi, na panguseni kwa [kupaka maji] vichwa vyenu na miguu yenu hadi vifundoni.”[1]

Maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَأَرْجُلَكُمْ

“… na miguu yenu…”

inaweza kusomwa kwa visomo viwili vilivyosihi kutoka kwa Mtume wa Allaah:

Cha kwanza:

وَأَرْجُلَكُمْ

“… na miguu yenu…”

Katika hali hii miguu yenu وَأَرْجُلَكُمْ ni mwongezo wa mashirikiano ya nyuso zenu وُجُوهَكُمْ, hivyo ina maana ya kwamba inatakiwa kuoshwa.

Cha pili:

وَأَرْجُلِكُمْ

“… na miguu yenu…”

Katika hali hii miguu yenu وَأَرْجُلِكُمْ ni mwongezo wa mashirikiano ya vichwa vyenu بِرُؤُوسِكُمْ, ikiwa na maana ya kwamba inatakiwa kupanguswa.

Sunnah ndio yenye kubainisha kama miguu inapaswa kuoshwa au kupanguswa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mwenye kuosha miguu yake pale ambapo inakuwa wazi na ikiwa amevaa soksi za ngozi alikuwa anafuta juu yake.

Ama kuhusiana na Sunnah, kitendo hicho kimepokelewa kwa mapokezi mengi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sihisi kigegezi chochote kuhusu kupangusa juu ya soksi za ngozi. Kwani kuna Hadiyth arobaini kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake juu ya hilo.”

Mshairi amesema:

Miongoni mwa Hadiyth zilizopokelewa kwa njia nyingi ni “Mwenye kusema uongo”

“Mwenye kujenga msikiti kwa ajili ya Allaah na akatarajia malipo”

Kuonekana kwa Allaah [Aakhirah], uombezi na Hodhi

Kupangusa juu ya soksi za ngozi na nyenginezo

Hizi ndio dalili za kupangusa katika Qur-aan na Sunnah.

[1] 05:06

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/157-158)
  • Imechapishwa: 27/04/2021