01. Ibn ´Abdil-Wahhaab anaitakidi yale wanayoitakidi Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema katika barua yake kwenda kwa watu wa al-Qaswiym wakati walipomuuliza kuhusu ´Aqiydah yake:

Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Namshuhudisha Allaah, Malaika Wake walio mbele yangu na nawashuhudisha kwamba mimi naitakidi yale wanayoitakidi kundi lililookoka; Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

MAELEZO

Namshuhudisha Allaah… – Ni kama kwamba haya yamechukuliwa kutoka katika maneno Yake (Ta´ala):

شَهِدَ اللَّهُ أَنَّهُ لا إِلَهَ إِلا هُوَ وَالْمَلائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِماً بِالْقِسْطِ لا إِلَهَ إِلا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Allaah Ameshuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye na Malaika, na wenye elimu [wote wameshuhudia kwamba Yeye] ni Mwenye kusimamisha [uumbaji Wake] kwa uadilifu – hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye; Mwenye nguvu zisizoshindikana, Mwenye hekima.”[1]

Yeye anamshuhudisha Allaah (Jalla wa ´Alaa), anawashuhudisha Malaika Wake na anawashuhudisha vilevile wanachuoni juu ya ´Aqiydah yake na kwamba hakuja na kitu kipya au kuibadilisha dini ya Allaah, kama inavosemwa juu yake. Si vyenginevyo isipokuwa amekuja na haki ya wazi.

Mimi naitakidi yale wanayoitakidi kundi lililookoka – ´Aqiydah ya kundi lililookoka ni lile ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

”Ummah huu utafarikiana katika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu. ” Wakasema: ”Ni lipi?” Akasema: ”Ni wale wataokuwa katika mfano wa yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah zangu.”[2]

[1] 03:18

[2] at-Tirmidhiy katika ”as-Sunan” yake (2641), al-Haakim katika “al-Mustadrak” yake (01/129) na wengineo kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aaasw (Radhiya Allaahu ´anh).

Vilevile ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (15/125 nambari. 6731), Abu Daawuud katika “as-Sunan” yake (4596) na wengineo kupitia kwa Abu Hurayrah  (Radhiya Allaahu ´anh).

Vilevile imekuja kutoka katika kundi la Maswahabah wengine wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tazama “as-Sunnah” ya Ibn Abiy ´Aaswim (63-69).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-ul-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 16/11/2020