01. Hadiyth “Swalah ya mtu katika mkusanyiko ni bora… “

297 – Abu Hurayrah (Rahdiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

صلاةُ الرجلِ في الجماعة تُضعَّفُ على صلاتِهِ في بيتِهِ وفي سوقِهِ خمساً وعشرين درجة، وذلك أنّه إذا توضأ فأحسنَ الوضوءَ، ثم خرج إلى المسجد لا يُخرِجه إلا الصلاةُ، لم يخطُ خُطوةً إلا رُفِعَت له بها درجةٌ، وحُطَّ عنه بها خطيئةٌ، فإذا صلّى لم تزل الملائكة تُصلّي عليه، ما دام في مصلاّهُ: اللهم صلِّ عليه، اللهم ارْحَمْه، ولا يزالُ في صلاةٍ ما انتظرَ الصلاةَ

“Swalah ya mtu katika mkusanyiko ni bora kuliko swalah yake nyumbani kwake na mahali pake anapofanyia biashara mara ishirini na tano. Hivyo ni kwa sababu anapotawadha na akaufanya vizuri wudhuu´ wake, kisha akatoka kuelekea msikitini na hakuna kingine kilichomtoa isipokuwa ni swalah, basi hatopiga hatua yoyote isipokuwa atanyanyuliwa kwayo ngazi na kufutiwa dhambi. Pindi anaposwali basi Malaika hawatoacha kuendelea kumuombea du´aa muda wa kuwa yuko hapo mahali pa kuswalia: “Ee Allaah! Msifu! Ee Allaah! Mrehemu!” Bado yuko ndani ya swalah muda wa kuwa anasubiri swalah.”[1]

Imekuja katika tamko lingine:

اللهمّ اغفر له، اللهم تُبْ عليه؛ ما لم يؤذِ فيه، ما لم يُحدِثْ فيه

“Ee Allaah! Mghufurie! Ee Allaah! Msamehe!” Muda wa hajaudhi humo, muda wa kuwa hajapatwa na hadathi humo.”

Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah, kwa kifupi, na Maalik katika “al-Muwattwa” kwa tamko lisemalo:

مَن توضّأ فأحسنَ الوضوءَ، ثم خرج عامداً إلى الصلاةِ، فإنّه في صلاةٍ ما كان يَعمِدُ إلى الصلاةِ، إنّه يُكتَبُ له بإحدى خُطوَتيْهِ حسنةٌ، وُيُمحَى عنه بالأخرى سيئةٌ، فإذا سمعَ أحدُكم الإقامةَ فلا يسْعَ، فإنَّ أعظمَكم أجراً أبعدُكم داراً “، قالوا: لِمَ يا أبا هريرة؟ قال:” مِنْ أجلِ كثرةِ الخُطا

“Yule mwenye kutawadha, akaufanya vizuri wudhuu´ wake, kisha akakusudia kutoka kwenda kuswali, basi yuko katika swalah muda wa kuwa ameikusudia swalah. Kwa kila hatua anayopiga anaandikiwa jema moja na kwa hatua nyingine anayopiga anafutiwa dhambi. Akisikia mmoja wenu adhaana, basi afanye haraka. Hakika yule miongoni mwenu mwenye ujira mkubwa ni yule anayeishi mbali zaidi.” Wakasema: “Kwa nini, ee Abu Hurayrah?” Akasema: “Kutokana na wingi wa hatua anazopiga.”

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake kwa tamko lisemalo:

مِن حينَ يخرجُ أحدُكم من منزله إلى مسجدي، فَرِجْلٌ تَكتُبُ له حسنةً، ورِجْل تَحُطُّ عنه سيئةً، حتى يرجعَ

“Kuanzia pale mmoja wenu anapotoka katika nyumba yake kuelekea msikitini. Kila hatua anayopiga anaandikiwa jema moja, na hatua nyingine anafutia dhambi – mpaka pale atakaporejea.”

Ameipokea an-Nasaa´iy na al-Haakim amepokea mfano wake bila ziada inayosema “mpaka pale atakaporejea”. al-Haakim amesema:

“Swahiyh juu ya sharti za Muslim.”[2]

Hapo kabla kumetangulia Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

إذا توضّأ أحدكم في بيته ثم أتى المسجدَ؛ كان في صلاةٍ حتّى يرجعَ

“Mmoja wenu atakapotawadha nyumbani kwake kisha akaja msikitini, basi anakuwa katika swalah mpaka atakaporejea.”[3]

[1] Swahiyh.

[2] adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Mambo ni kama walivosema.

[3] Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/239-240)
  • Imechapishwa: 02/12/2022
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy