01. Hadiyth “Hakika wawili hawa wanaadhibiwa na hawaadhibiwi… “

157 – Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita karibu na makaburi mawili na akasema: “Hakika wawili hawa wanaadhibiwa na hawaadhibiwi kwa jambo kubwa. Lakini hata hivyo ni jambo kubwa. Kuhusu mmoja wao alikuwa akitembea na kueneza umbea na mwengine alikuwa hajichungi na mkojo wake.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy ambaye ni upokezi wake, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah. Katika upokezi mwingine wa al-Bukhaariy na Ibn Khuzaymah katika “as-Swahiyh” yake imekuja:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita karibu na ukuta miongoni mwa kuta za Makkah au Madiynah ambapo akaskia sauti za watu wawili wanaoadhibiwa ndani ya makaburi yao. Akasema: “Hakika wawili hawa wanaadhibiwa na hawaadhibiwi kwa jambo kubwa. Lakini hata hivyo ni kubwa. Kuhusu mmoja wao alikuwa hajichungi na mkojo wake na mwengine alikuwa akitembea na kueneza umbea.”

al-Bukhaariy ameiweka Hadiyth hiyo kichwa cha khabari kinachosema:

“Miongoni mwa madhambi makubwa ni mtu kutojichunga na mkojo wake.”

al-Khattwaabiy amesema:

“Hawaadhibiwi kwa jambo kubwa maana yake ni kwamba hawakuadhibiwa kwa jambo ambalo lilikuwa ni kubwa kwao au ilikuwa ni vigumu kujiepusha nalo. Hamaanishi kuwa dhambi hiyo yenyewe kama yenyewe sio kubwa kwa upande wa dini na kwamba ni nyepesi.”[2]

Kutokana na kuchelea kwake watu wasije kufahamu makosa ndipo yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasahihisha na kusema:

“Lakini hata hivyo ni kubwa.”

Na Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] Swahiyh.

[2] Ma´aalim-us-Sunan (1/27).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/176)
  • Imechapishwa: 05/04/2021
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy