00. Jilbaab ni lazima ifunike mwili mzima isipokuwa yale yaliyovuliwa

Jilbaab ni lazima ifunike mwili mzima isipokuwa yale yaliyovuliwa. Dalili ya hili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika [kwa kuwa hakuna njia ya kuyaficha]; hivyo waangushe khimari zao mpaka vifuani mwao. Na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, baba zao, baba za waume wao, wana wao wa kiume, wana wa kiume wa waume zao, kaka zao, wana wa kiume wa kaka zao, wana wa kiume wa dada zao, wanawake wao [dada zao wa Kiislamu], wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, watumishi wanaume wasio na matamanio [tena kwa wanawake], au watoto ambao [bado] hawaelewi [kitu kuhusu] yanayohusu uke. Na wala wasipige miguu yao [wanapotembea] yajulikane yale wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini ili mpate kufaulu!”[1]

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

“Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako – na wanawake wa waumini – wajiteremshie Jilbaab zao; hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[2]

Aayah ya kwanza ni dalili ya wazi kwamba mapambo yote ni lazima yafunikwe mbele ya wanaume ambao ni ajinabi isipokuwa yale yenye kuonekana pasi wao kukusudia. Katika hali hiyo wanawake hawapati dhambi juu ya hilo maadamu ni mwenye kutilia bidii kuyafunika. Haafidhw Ibn Kathiyr amesema:

“Bi maana wasiwaonyeshe kitu katika mapambo wanaume ajinabi, isipokuwa yale ambayo hakuna namna ya kuyafichika. Ibn Mas´uud amesema:

“Kama ile nguo inayovaliwa juu ya na mavazi.”

Kwa msemo mwingine ni ile shuka ambayo wanawake wa kiarabu walikuwa wakivaa juu ya mavazi pamoja vilevile na yale yenye kuonekana ndani ya nguo. Hawapati dhambi kwa hilo kwa sababu hiki ni kitu ambacho hakiwezi kufichika.”

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Niliona shanga ya mguuni ya ´Aaishah bint Abiy Bakr na Umm Sulaymaan wakati walipokuwa wakiharakisha kubeba maji migogoni mwao na kuwapa watu… “[3]

Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

“Hii ilikuwa kabla ya kufaradhishwa kujifunika. Inawezekana vilevile yalitokea pasi na kukusudia.”

Hii ndio tafsiri ya:

إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“… isipokuwa yale yanayodhihirika… “

Hivyo ndivo unaashiria mtiririko wa Aayah katika nafasi ya kwanza.

[1] 24:31

[2] 33:59

[3] al-Bukhaariy (7/290) na Muslim (5/197).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 39-40
  • Imechapishwa: 07/11/2017