Kwa msemo mwingine katika Aayah hakuna dalili juu ya kwamba uso wa mwanamke ni uchi ambao ni lazima kuufunika. Kubwa lililotajwa ni yeye kujiteremshia jilbaab juu yake. Amri, kama unavoona mwenyewe, ni yenye kuachiwa. Kuna uwezekano vilevile ikawa na maana ya kufunika mapambo yote asiyotakiwa kuyaonyesha, kama yalivosemwa wazi hayo katika ile Aayah ya kwanza, na hivyo majulisho yatakuwa yameanguka. Kuna uwezekano vilevile ikawa na maana yenye kuenea zaidi kuliko hivo na hivyo kukaingia uso pia. Wanazuoni waliotangulia wameonelea maoni yote mawili na Ibn Jariyr akayanukuu katika ”Jaamiy´-ul-Bayaan” na pia as-Suyuutwiy katika ”ad-Durr al-Manthuur”. Sioni kama kuna faida kubwa kuyanukuu hapa na nitatosha kuyaashiria. Yule anayetaka kuyasoma basi arejee huko.

Naona kuwa maoni ya kwanza ndio ya haki zaidi kutokana na sababu zifuatazo:

1 – Qur-aan inajifasiri yenyewe kwa yenyewe. Katika Aayah ya ”an-Nuur” iliyotangulia imebainika kuwa uso sio lazima kuufunika. Kwa hivyo kujiteremshia katika ”al-Ahzaab” kunalenga kila kitu isipokuwa uso kwa ajili ya kuoanisha kati ya Aayah hizo mbili.

2 – Sunnah inaibainisha Qur-aan na kuyafanya maalum yale yaliyokuja kwa njia ya kuenea. Zipo Hadiyth nyingi zinazoonyesha kuwa uso sio lazima kuufunika na kwa ajili hiyo ikalazimika kuifasiri Aayah katika ”al-Ahzaab” kutokana nazo.

Kwa hivyo ikathibiti kuwa uso wa mwanamke sio uchi unaotakiwa kufunikwa. Isitoshe ndio maoni ya kikosi cha wanazuoni wengi, kama alivosema Ibn Rushd katika ”Bidaayat-ul-Mujtahid”. Miongoni mwao ni Abu Haniyfah, Maalik na ash-Shaafi´iy. Hata Ahmad katika moja ya maoni yake, kama ilivyotajwa katika ”al-Majmuu´”. Kwa mujibu wa at-Twahaawiy maswahiba wawili wa at-Twahaawiy wana mtazamo huo. Katika kitabu cha Shaafi´iyyah ”al-Muhimmaat” imesemwa kuwa maoni hayo ndio ya sawa, kama alivotaja Shaykh ash-Sharbiyniy katika ”al-Iqnaa´”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 87-89
  • Imechapishwa: 19/09/2023
Takwimu
  • 25
  • 413
  • 1,821,444