00 – Dibaji ya Uislamu ndio dini kamilifu

Himdi zote njema zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, familia yake, Maswahabah zake na wale wenye kuita katika ulinganizi wake mpaka siku ya Qiyaamah.

Ama baada ya hayo;

Huu ni muhadhara niliotoa kwenye msikiti wa Mtume kutokana na ombi la mfalme wa Marocco. Baada ya hapo baadhi ya ndugu zangu wakanitaka kuuandaa ili kuueneza. Nikawakubalia maombi yao kwa kutarajia Allaah atanufaisha kwao.

Allaah (Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu.”[1]

Siku hiyo ilikuwa ni siku ya ´Arafah. Ilikuwa ni siku ya ijumaa katika hajj ya kuaga. Aayah hii tukufu iliteremshwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesimama ´Arafah. Baada ya kuteremshwa, aliishi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku thamanini na moja.

Katika Aayah hii tukufu Allaah (Ta´ala) ameweka wazi kwamba ametukamilishia dini yetu. Hatoipunguza kamwe na wala haitohitajia nyongeza. Kwa ajili hiyo ndio maana amefanya utume kumalizika kwa Mtume wetu – swalah na amani ziwaendee wote.

Kadhalika ameweka wazi ya kwamba ameridhia kwetu Uislamu ndio iwe dini yetu. Ina maana ya kwamba hatokasirika kwa hilo kamwe. Kwa ajili hiyo ndio maana amesema kuwa hatoikubali dini nyingine. Amesema:

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake; naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[2]

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

“Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.”[3]

Kujengea juu ya kwamba dini imekamilika na hukumu zote ziko waziwazi, ndio kunafikiwa neema zote katika maisha haya na huko Aakhirah. Ndio maana Amesema:

وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي

“… na Nimekutimizieni neema Yangu.”[4]

Katika Aayah hii tukufu kuna dalili ya wazi juu ya kwamba Uislamu haukuacha kitu chochote ambacho viumbe wanahitaji duniani wala Aakhirah, isipokuwa imekiweka wazi na kukibainisha.

Tutatoa baadhi ya mifano juu ya hilo. Kutabainishwa mambo kumi makubwa ambayo dunia hii inazunguka juu yake. Mambo hayo yanawahusu walimwengu duniani na Aakhirah.

La kwanza: Tawhiyd.

La pili: Mawaidha.

La tatu: Tofauti kati ya matendo mema na matendo mabaya.

La nne: Kuhukumu kwa isiyokuwa Shari´ah Tukufu.

La tano: Hali ya jamii.

La sita: Uchumi.

La saba: Siasa.

La nane: Nguvu za makafiri juu ya waislamu.

La tisa: Idadi dhaifu ya waislamu na udhaifu wa nguvu za kijeshi ukilinganisha na za makafiri.

La kumi: Jamii kutofautiana nyoyo.

Tutayaangalia matatizo yote haya kupitia Qur-aan.

[1] 05:03

[2] 03:85

[3] 03:19

[4] 05:03

  • Mhusika: Imaam Muhammad Amiyn ash-Shanqiytwiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Islaam diyn al-Kaamil, uk. 7-8
  • Imechapishwa: 13/06/2023