Zayd al-Madkhaliy kuhusu maneno ya al-Hajuuriy kwamba Ahl-us-Sunnah ndio walio karibu zaidi na haki

Aliulizwa Shaykh na ´Allaamah Zayd al-Madkhaliy (Rahimahu Allaah):

Ni yapi maoni yako kwa mwenye kusema kuwa Ahl-us-Sunnah ndio kundi lililo karibu zaidi na haki?[1] Je, ni sahihi au batili?

Jibu: Hapana, si sahihi. Ahl-us-Sunnah ndio watu wa haki. Lakini hata hivyo hawakukingwa na kutumbukia katika makosa na kwenda kinyume mambo ambayo hayawatoi katika njia ya waumini. Mtu wa Sunnah anapokosea anajirudi katika haki na anaacha kosa na pia anamuomba Allaah msamaha kutokamana na dhambi yake. Kukingwa na makosa ni kwa Mitume na Manabii watukufu peke yao na si wengine. Kwa hivyo ibara hiyo si sahihi.

Hakusemwi kuwa Ahl-us-Sunnah ndio kundi liliflo karibu zaidi na haki. Bali inatakiwa kusemwa kwamba Ahl-us-Sunnah ndio watu wa haki. Hili halipelekei kwamba hawakosei na wala hawatumbukii katika kwenda kinyume. Ni mamoja wawe wamefanya hivo kwa kutokujua au kwa kujua. Wala hilo haliwatoi kuwa Ahl-us-Sunnah.

[1] al-Hajuuriy amesema katika mkanda “Tabyiyn al-Kadhib wal-Yamiyn”:

“Mtu huyu anasema kwamba sisi tunasema kuwa kundi lililo karibu zaidi na haki [ni Ahl-us-Sunnah]. Haya sio maneno yetu sisi tu. Haya ni maneno ya mwalimu wetu pia na yametajwa na yanajulikana kutoka kwake. Wanayajua wanafunzi wake watukufu na sio mtu kama wewe uliyeanguka.”

  • Mhusika: Shaykh ´Arafaat bin Hasan bin Ja´far al-Muhammadiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Bayaan al-Fawriy (01/19)
  • Imechapishwa: 11/10/2016