Zakaah nje ya nchi


Swali: Je, inajuzu kutoa zakaah kutoka Saudi Arabia kwenda Sudan? Kwani mimi hii leo nafanya kazi Saudi Arabia na hutuma zakaah yangu kwenda huko.

Jibu: Ndio, inafaa kutoa zakaah kutoka Saudi Arabia kwenda Sudan au nchi nyenginezo za waislamu au kwa muislamu yeyote mwenye kuistahiki mahali popote ulimwenguni. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Hakika si venginevyo zakaah ni kwa ajili ya mafakiri na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao [kwa ajili ya Uislamu] na kuwakomboa mateka na wenye deni na katika njia ya Allaah na msafiri [aliyeharibikiwa] – ni faradhi itokayo kwa Allaah; na Allaah ni Mjuzi, Mwenye hekima.”[1]

Mahali popote watapatikana watu hawa basi ndio wanaostahiki kupewa zakaah. Isipokuwa lililo bora zaidi ni mtu aitoe katika ile nchi inayopatikana mali hiyo. Kwa sababu nchi ambayo mali hiyo ipo watu wake ndio wenye haki nayo zaidi. Kwa ajili hiyo haitakiwi kuwanyima nayo na kuipeleka mbali na wao. Isipokuwa kama kuna manufaa kuitoa zakaah hiyo kwenda nchi nyingine. Pengine kwa sababu hao walioko katika nchi nyingine ni ndugu wa huyo anayetoa zakaah, wahitaji zaidi au sababu nyenginezo.

[1] 09:60

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (19) http://binothaimeen.net/content/6839
  • Imechapishwa: 15/09/2021