Zakaah juu ya pesa iliyokusanywa kwa ajili ya kujenga msikiti

Swali: Tumekusanya kiwango fulani cha pesa kwa ajili ya kujenga msikiti. Je, tutoe zakaah kikifikiwa na mwaka na hatujaanza kujenga kwa sababu ya kutokamilika kiwango tunachotaka?

Jibu: Hakina zakaah. Zakaah imeshurutishwa iwe na mmiliki maalum. Msikiti hauna mmiliki maalum. Hiki ni kitendo cha kheri watu wamejitolea kukusanya kwa ajili ya kujenga msikiti au kituo cha kuhifadhi Qur-aan na mfano wake. Pesa kama hiyo haitolewi zakaah.

Lakini ikiwa mtu anakusanya pesa inayotokana na mali yake kwa ajili ya kufanya kitendo cha kheri na hajaitoa mpaka sasa, basi anatakiwa kuitolea zakaah mpaka pale atapoitoa nje. Haijuzu kwake kusema atatoa baadaye kwa njia ya kwamba akanuia hivi sasa kwamba ataitoa kisha akafanya hivo baadaye. Muda wa kuwa hajaitoa na pesa bado iko kwake, basi aitolee zakaah mpaka pale atapoitoa nje ya akaunti.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (21)
  • Imechapishwa: 03/09/2021