Yafahamu haya utafumbukiwa na utatizi mwingi

172- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Siku ya Qiyaamah Allaah atasema kumuuliza mtu ambaye atakuwa na adhabu nyepesi kabisa Motoni: “Ee mwanadamu! Unasemaje juu ya makazi yako?” Atasema: “Makazi yenye shari kabisa.” Amwambie: “Lau ungemiliki dunia na vyote vilivyomo ndani yake ungelitoa fidia kwavyo?” Aseme: “Ndio.” Ndipo atasema: “Umesema uongo! Nilitaka kwako jambo ambalo ni jepesi zaidi kuliko hayo kipindi ambacho ulikuwa mgongoni mwa Aadam: usinishirikishe Mimi na chochote na hivyo Sintokuingiza Motoni.  Lakini hukutaka jengine isipokuwa shirki.” Ndipo kuamrishwe aingizwe Motoni.”[1]

an-Nawawiy amesema:

“Lau tungekurudisha duniani basi usingeyatoa fidia. Kwa sababu ulitakwa jambo jepesi kuliko hayo lakini ukakataa. Hivyo yanaingia ndani ya maana ya maneno Yake (Ta´ala):

وَلَوْ رُدُّوا لَعَادُوا لِمَا نُهُوا عَنْهُ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ

“Lau wangelirudishwa, kwa hakika wangeyarudia yale waliyokatazwa na hakika wao ni waongo.” (06:28)

Kwa ajili hiyo maana ya Hadiyth hii inaoana na maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ أَنَّ لَهُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لِيَفْتَدُوا بِهِ مِنْ عَذَابِ يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَا تُقُبِّلَ مِنْهُمْ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Hakika wale waliokufuru, lau watakuwa na vile vyote vilivyomo ardhini na vyenginevyo mfano kama hivyo, ili watoe fidia kwavyo kuepukana na adhabu ya siku ya Qiyaamah, hayatokubaliwa kutoka kwao, na watapata adhabu iumizayo.” (05:36)

Maneno Yake:

“Nilitaka kwako… “

Bi maana nilipenda kutoka kwako. Wakati fulani matakwa katika Shari´ah hutajwa kwa njia ya kuachia na kukakusudiwa yale yenye kuenea kheri na shari, uongofu na upotevu. Mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن يُرِدِ اللَّـهُ أَن يَهْدِيَهُ يَشْرَحْ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ ۖ وَمَن يُرِدْ أَن يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقًا حَرَجًا

“Basi yule ambaye Allaah anataka kumwongozoa, kumkunjulia kifua chake kwa Uislamu. Na yule ambaye Anataka kumpotoa, hukifanya kifua chake kuwa na dhiki chenye kubana.” (6:125)

Haya ni matakwa ambayo lazima yatendeke.”

Wakati mwingine matakwa hutajwa kwa njia ya kuachia na kukakusudiwa kupenda na kuridhia. Mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

“Allaah anakutakieni mepesi na wala hakutakieni mazito.” (02:185)

Maana hii ndio makusudio ya maneno Yake (Ta´ala) katika Hadiyth:

“Nilitaka kwako jambo ambalo ni jepesi zaidi kuliko hayo kipindi ambacho ulikuwa mgongoni mwa Aadam… “

Bi maana Nilipenda kutoka kwako. Matakwa kwa maana hii yanaweza yasitimie. Kwa sababu Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) hamlazimishi yeyote juu ya kumtii ingawa amewaumba viumbe kwa lengo hilo:

فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ

“ Hivyo yule anayetaka aamini na yule anayetaka akufuru.” (18:29)

Kutokana na hayo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anaweza kutaka mja Wake afanye kitu asichokipenda na akapenda mja afanye kitu asichokitaka. Matakwa haya Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) huyaita kuwa ni ´matakwa ya kilimwengu` kujengea juu ya maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

”Hakika amri Yake anapotaka chochote hukiambia: “Kuwa!” nacho huwa.” (36:82)

Sambamba na hilo yale matakwa mengine yanayoenda sambamba na kuridhia Kwake huyaita kuwa ni ´matakwa ya Kishari´ah`. Yule ambaye atafahamu mgawanyiko huu basi atafumbukiwa na utatizi mwingi unaofungamana na mipango na makadirio na pia kusalimika kutokamana na fitina ya fikira za Jabriyyah na Mu´tazilah. Upambanuzi wa hayo uko katika kitabu kitukufu ”Shifaa’-ul-´Aliyl” cha Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah).

[1] al-Bukhaariy (2/333) na Muslim (8/134).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (1/1/332-334)
  • Imechapishwa: 20/04/2020