Ya kuzingatia pindi mwanamke amedharurika kwenda kwa daktari wa kiume

Swali: Vipi kuhusu jambo linalowasumbua watu wengi ambalo suala la mwanamke na daktari wa kiume? Kipi unachowanasihi kina dada wa Kiislamu juu ya jambo hili.

Jibu: Hapana shaka kwamba suala la mwanamke na daktari wa kiume ni suala muhimu. Ukweli wa mambo ni kwamba linachosha sana. Lakini Allaah akimruzuku mwanamke uchaji na umaizi basi anachunga na kutilia umuhimu jambo hili. Haifai kwa mwanamke kukaa faragha na daktari wa kiume kama ambavo haifai kwa daktari wa kiume kukaa faragha na mwanamke. Kumetoka maagizo na mafunzo yanayokataza jambo hilo kutoka kwa watawala. Kwa hiyo ni lazima kwa mwanamke kulipa umuhimu jambo hili na ajibidishe kuwatafuta madaktari wa kike. Wakipatikana ni vizuri na hivyo kutakuwa hakuna haja ya kwenda kwa daktari wa kiume.

Haja ikipelekea kwenda kwa daktari wa kiume kwa sababu ya kutopatikana madaktari wa kike, basi hakuna neno kujifunua na kutibiwa wakati wa haja. Haya ni miongoni mwa mambo ambayo yanafaa wakati wa haja. Lakini kujifunua kusiambatane na kukaa naye chemba. Bali kupitike pamoja na kuwepo kwa Mahram wa mwanamke huyo au mume wake ikiwa inahusiana na kujifunua kwa viungo vya juujuu kama mfano wa kichwa, mikono, mifuu na mfano wake. Ikiwa kujifunua kunahusiana na sehemu za siri basi mwanamke awe pamoja na mumewe akiwa amekwishaolewa au awe pamoja na mwanamke mwenzie. Kufanya hivi ndivo bora na salama zaidi. Pia anaweza kuwa muuguzi wa kike au wauguzi wawili wa kike waliohudhuria pale. Lakini iwapo atakuwa na mwanamke mwingine asiyekuwa muuguzi wa kike basi kitendo hicho ndicho kitakuwa bora na salama zaidi kutokamana na mashaka. Kuhusu kukaa naye chemba ni jambo halifai.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/392)
  • Imechapishwa: 24/06/2020